📌Silaha 105 zakamatwa, mitego ya nyaya 10,971 yateguliwa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeimarisha mapambano dhidi ya ujangili kwa kufanya doria 301,314 katika hifadhi za taifa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatua iliyowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 30,559 na kuongeza idadi ya wanyamapori adimu.
Hatua hiyo imewezwaha kuongezeka kwa idadi ya faru kutoka 128 mwaka 2021 hadi wanaokadiriwa kufikia 170 mwaka 2026.

Mafanikio hayo ni sehemu ya hatua mbalimbali za uhifadhi zilizotekelezwa na Shirika hilo, ambazo pia zimehusisha kuimarisha ulinzi wa wanyamapori, kurejesha mifumo ikolojia na kudhibiti matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo leo Novemba 10,2026, Kamishna wa TANAPA, Massana Mwishawa amesema katika kipindi hicho Shirika lilifanya doria 301,314 kati ya doria 314,940 zilizopangwa, zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 30,559 katika matukio 25,006 ya ujangili.

Amesema katika operesheni hizo pia mifugo 65,860 iliyokuwa imeingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria ilikamatwa, silaha 105 zilikamatwa na mitego ya nyaya 10,971 iliteguliwa katika maeneo ya hifadhi.
Katika mafanikio mengine ya uhifadhi, amesema idadi ya sokwe waliozoeshwa imeongezeka kutoka 196 mwaka 2021 hadi 288 mwaka 2026, huku mbwa mwitu 12 wakiwa katika eneo la uzalishaji katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi na wengine 25 wakiachiliwa kwenda katika maeneo yao ya asili.

Amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa ndege nyuki (drones) 40 kwa ajili ya doria za anga na ufuatiliaji wa wanyamapori, huku TANAPA ikijenga vituo vitatu vya kisasa vya mawasiliano na minara 10 ya redio katika Hifadhi za Taifa Serengeti, Ziwa Manyara, Tarangire na Mkomazi.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yamesaidia kutambua makundi ya tembo kabla hayajafika katika maeneo ya wananchi na kuwawezesha askari kuyaelekeza kurudi ndani ya hifadhi.

Katika kipindi hicho, matukio 9,787 ya wanyamapori wakali na waharibifu yalizuiwa kabla ya kusababisha athari kwa wananchi.