
Na Mwandishi Wetu, Arusha
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu amechaguliwa na Baraza la Uongozi la Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja huo unaofanyika jijini Dodoma.
Uchaguzi huo umefanyika wakati wa Mkutano wa Baraza la Uongozi la IPU uliofanyika katika moja ya ukumbi kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), leo Oktoba 6, 2026.
Mheshimiwa Spika amependekezwa na Spika wa Bunge la Wawakilishi la Uingereza (House of Commons) Sir Lindsay Hoyle na kuungwa mkono na Spika kutoka Falme za Kiarabu na Bunge la Uganda.
Akitoa hoja ya kumpendekeza Mheshimiwa Zungu, Sir Lindsay Hoyle amesema anayo heshima kupendekeza jina la Spika wa Bunge la Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Arusha (AICC).
“Ninayo heshima kumpendekeza Spika wa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), naweza kusema urafiki wa muda mrefu, urafiki wenye mizizi, ndiyo maana kwa heshima kubwa nampendekeza Spika wa Tanzania.
Akitoa salamu za shukrani, Mheshimiwa Zungu alishukuru kwa kuchaguliwa na kueleza kwamba amekubali kushika nafasi hiyo kwa moyo mmoja.
“Mheshimiwa Rais wa IPU na wajumbe wote wa Mkutano huu, kwa moyo wa dhati, nawashukuru wajumbe wote, Tanzania inajivunia kuwakaribisha jijini Arusha na tutaendelea kuwa pamoja katika mkutano huu wa 153 wa IPU” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa IPU na Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania alimpongeza Mheshimiwa Zungu kuwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano huo wa 153 wa IPU.


