
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WITO umetolewa kwa vijana nchini wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 kujitokeza kushiriki kutoa mawazo bunifu ya katika shindano la Kitaifa la wazo bunifu ’Mashindano Vijana Uchumi Chalenji’
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Vijana Uchumi Chalenji’, Joseph Brighton Malekela, ametangaza rasmi kuanza kwa shindano la wazo bora la kiuchumi linalolenga kuibua ubunifu wa vijana katika kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, kuhusu shindano hilo lenye kauli mbiu “Wana tunafikiri, Taifa linasonga”, Malekela alisema lengo kuu ni kuwapa vijana jukwaa la kuonesha mawazo yao ya kibunifu yenye uwezo wa kutatua changamoto za kiuchumi na kuongeza fursa za ajira.
Ameeleza kuwa, washiriki wanatakiwa kuwa vijana wa Kitanzania na kila mshiriki atawasilisha wazo lake kwa maandishi yasiyozidi maneno 300 pamoja na video isiyozidi dakika tatu.
Amebainisha kuwa vigezo vitakavyotumika kuchagua washindi ni pamoja na ubunifu na upekee wa wazo, uelewa wa changamoto za kiuchumi za kimataifa, uwezo wa wazo kutekelezeka, mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa pamoja na uwezo wa kuongeza fursa kwa vijana. pia, ubora na uwazi wa uwasilishaji vitazingatiwa.
Kwa mujibu wa Malekela, mchakato wa ushindani utaanza na mchujo wa awali ambapo washiriki 100 bora watachaguliwa na kupatiwa taarifa.
Washiriki hao watapata fursa ya kushiriki mafunzo maalum kabla ya kuwasilisha tena mawazo yao mbele ya majaji katika hatua ya robo fainali.
Ameongeza kuwa washiriki 30 wataingia hatua ya nusu fainali ambapo watapata nafasi ya kuboresha mawazo yao na mipango ya utekelezaji.
“Hatua ya mwisho itahusisha washindi 10 bora ambao wataandaliwa tukio kubwa pamoja na kupatiwa mafunzo ya ziada ya kuboresha na kuwasilisha mawazo yao kitaalamu,” amesema.
Kuhusu zawadi, Malekela amesema jumla ya Sh. milioni 50 zimetengwa ambapo mshindi wa kwanza atapata Sh. milioni 30, wa pili milioni 15 na wa tatu milioni 5.
“Washindi wote 10 bora watapatiwa Sh. milioni 1 kila mmoja pamoja na fursa ya ‘mentorship’ ili kukuza mawazo yao,” amesisitiza.
Aidha, washiriki 30 bora wataunganishwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza miradi yao huku washiriki 100 watakaofika hatua ya awali wakitambuliwa kwa vyeti.
Malekela amesisitiza kuwa kamati itaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari ili kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shindano hilo, ambalo linatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Mei mwaka huu.