
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imeitaka Tume ya Ushindani (FCC) kuimarisha na kupanua matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi na ufutiliaji wa udhibiti wa bidhaa bandia katika masoko ya kidijitali. Aidha, FCC imetakiwa kuongeza kasi ya uratibu na ushirikiano wa karibu na taasisi zingine za udhibiti, ikiwamo vyombo vya dola na mamlaka za forodha, ili kuhakikisha taarifa zinashirikishwa kwa wakati na hatua zinachukuliwa haraka dhidi ya bidhaa bandia.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alitoa maelekezo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia 2026 yaliyofanyika Juni 25 jijini Dar es Salaam. Katika maadhimisho hayo, Mapunda aliwataka wadau na FCC kuimarisha elimu kwa umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia kupitia kampeni za kitaifa zinazolenga kuwafikia watumiaji wa mwisho wa bidhaa, wakiwamo wafanyabiashara na makundi maalumu.
Kadhalika, aliitaka FCC kuendelea kujenga ushirikiano wa moja kwa moja na wamiliki wa alama za biashara na sekta binafsi ili kuboresha mifumo ya utambuzi wa bidhaa bandia na kurahisisha utoaji wa taarifa na ushahidi wa kitaalamu wakati wa uchunguzi. Mapunda alisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha uwezo wa rasilimali watu kupitia mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika uchunguzi, uendeshaji wa mashauri na utekelezaji wa sheria dhidi ya wahusika wa biashara za bidhaa bandia.
Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema maadhimisho ya mwaka huu yameandaliwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na wadau wote nchini, sambamba na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na makundi mbalimbali ili kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa bandia. Alibainisha kuwa katika operesheni za kudhibiti bidhaa bandia, FCC imefanikiwa kukamata viwanda bubu vya kuzalisha vinywaji na shehena kubwa ya sigara na vilainishi.
“Mapambano haya yanamaanisha kuwa walaji wapate bidhaa salama na kula bidhaa salama. Hivyo mkutano huu tumejikita kutengeneza mjadala wa kusaidia kulinda usalama wa watumiaji wa bidhaa,” alisema Khadija.
Naye Kamishna wa FCC, Said Tunda, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, alisema tume imeendelea kuimarisha mifumo ya kuhakikisha wanapambana kudhibiti bidhaa bandia na inatarajia kuongeza uwezo wa kuondoa bidhaa hizo kwa wakati. Aliongeza kuwa FCC itaimarisha ushirikiano na wamiliki wa alama za biashara, kuongeza elimu kwa umma na kuendeleza matumizi ya teknolojia katika shughuli za ukaguzi.
Kwa upande wake, Jaji Rose Ibrahim kutoka Baraza la Ushindani (FCT) alisema wanashirikiana na serikali kuhakikisha ushindani wa haki sokoni na kulinda haki za walaji. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote katika kuzuia uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bandia, huku akiwataka wananchi kuwa waangalifu kwa kuzingatia viashiria vya usalama na ubora wa bidhaa.
Tanzania imeadhimisha Siku ya Kitaifa ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia Juni 25, 2026, kwa kauli mbiu isemayo: “Linda Maisha na Masoko Dhidi ya Pombe, Vilainishi na Sigara Bandia”, ambapo maadhimisho hayo yametumika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za bidhaa bandia na kuimarisha juhudi za kitaifa na kimataifa za kupambana na biashara hiyo haramu.







