Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini

WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.29.09-1024x683 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI imeahidi kuimarisha ushirikiano na waagizaji na wasambazaji wa mafuta ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wingi na kwa wakati katika maeneo yote nchini.

Ahadi hiyo imetolewa leo Oktoba 3,2026 na Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, alipokutana na viongozi na wanachama wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati, jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalilenga kujenga ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mafuta, pamoja na kujadili namna ya kuboresha usimamizi na kukuza sekta hiyo nchini.

Katika kikao hicho, Dkt. Homera amesikiliza maoni na changamoto za wadau kuhusu uendeshaji na maendeleo ya sekta ya mafuta. Pande hizo pia zilijadili mikakati ya kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa uhakika katika maeneo yote ya nchi, ili kusaidia shughuli za kiuchumi na kijamii.

Dkt. Homera alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha usalama wa upatikanaji wa mafuta, akisisitiza kuwa mafuta ni nishati muhimu inayotegemewa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aliongeza kuwa mawasiliano na ushirikiano kati ya Serikali, waagizaji na wasambazaji ni muhimu katika kubaini na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza, na hivyo kuongeza ufanisi wa sekta na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Mafuta, Goodluck Shirima; viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, wakiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), pamoja na viongozi na wanachama wa TAOMAC.

WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.32.16-1024x683 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini
WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.31.57-1024x683 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini
WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.29.45-1024x683 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini
WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.29.24-1024x683 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini
WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.29.10-1024x511 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini
WhatsApp-Image-2026-10-03-at-08.29.09-1-1024x683 Serikali, TAOMAC Kuimarisha Upatikanaji wa Mafuta Nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *