Aagiza ukaguzi wa maduara, mabwawa ya tope sumu na mipango ya dharura kuimarishwa

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amewaagiza wamiliki, mameneja, wachimbaji wadogo na maafisa madini nchini kuchukua hatua za haraka kujiandaa na mvua kubwa za El ñino zinazotarajiwa kunyesha kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu.
Samamba ametoa agizo hilo leo, Septemba 28, 2026, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo.
Amesema kwa kuzingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa mvua kubwa kuliko wastani, migodi inapaswa kuongeza ukaguzi wa maduara, mabwawa ya kuhifadhia tope sumu (TSF), maeneo ya kuhifadhi miamba taka na miundombinu mingine.
“Wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuboresha taratibu za usalama ili ziakisi hali ya mvua kubwa, kuongeza ukaguzi wa maduara na mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, pamoja na kuhakikisha kila mgodi una mpango wa dharura unaoeleweka na kutekelezeka,” amesema.
Amesema mvua kubwa inaweza kusababisha kuporomoka kwa maduara na kuta za migodi, mafuriko ndani ya migodi, kudhoofika kwa mihimili inayoshikilia miamba na kujaa kwa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, hali inayoweza kuhatarisha maisha, mazingira na miundombinu.
Samamba amesisitiza kuwa hakuna mchimbaji anayepaswa kuingia au kuendelea kufanya kazi chini ya ardhi wakati wa mvua kubwa au mara baada ya mvua ikiwa eneo hilo si salama.
Ameagiza maduara yakaguliwe kila siku kabla ya kazi kuanza, maeneo dhaifu yaimarishwe, mifereji ijengwe na kusafishwa mara kwa mara na kila mgodi uwe na pampu za kuvuta maji pamoja na mafuta ya kutosha kwa matumizi ya dharura.
Kuhusu mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, amesema waendeshaji wanapaswa kuhakikisha yana nafasi na uimara wa kutosha kuhimili ongezeko la maji, huku ukaguzi wa kingo, mifereji, kiwango cha maji, uvujaji na mmomonyoko ukifanyika kwa wakati.
Aidha, amesisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za usalama wakati wa ulipuaji na kupanga zamu za wachimbaji kwa kuzingatia uwezo wa watendaji ili kupunguza uchovu na ajali.
Amewaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010 na kuchukua hatua pale ukiukwaji unapobainika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Migodi Tanzania, Shija Mussa, ameomba Serikali kusaidia upatikanaji wa mitambo mikubwa ya kunyonya maji (heavy-duty pumps), akisema maji kujaa kwenye mashimo ni moja ya changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wakati wa mvua.

Awali, Mkurugenzi wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Aziza Swedi, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wachimbaji uwezo wa kuchukua tahadhari mapema, akiwataka washiriki kurejea katika maeneo yao ya kazi, kubaini maeneo hatarishi na kurekebisha kasoro kabla madhara hayajatokea.



