Migogoro ya wawekezaji PPP kusikilizwa Kimataifa-Kafulila

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MABADILIKO ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yamefungua fursa kwa migogoro ya wawekezaji kusikilizwa katika taasisi za kimataifa za utatuzi wa migogoro ya uwekezaji, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter).

Kafulila amesema mwaka 2023 aliteuliwa na Rais kuwa Kamishna wa Ubia (PPP) chini ya Wizara ya Fedha, wakati huo ikiongozwa na Dkt. Mwigulu Nchemba, na kuelekezwa kusimamia mabadiliko ya Sheria ya PPP.

Amesema miongoni mwa mambo yaliyowekwa katika mabadiliko hayo ni kuruhusu migogoro ya wawekezaji kusikilizwa katika taasisi za kimataifa za utatuzi wa migogoro ya uwekezaji, ikiwemo International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID).

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kuimarisha mageuzi ya kisera, kisheria na kitaasisi.

Aidha, kauli hiyo inaendana na wito wa Waziri wa Fedha, Balozi Omary Khamis, kuhusu umuhimu wa kufanya mageuzi ya jumla katika namna ya kufikiri, kupanga na kuendesha uchumi ili kufikia malengo makubwa yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *