Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi
Hamad Yussuf Masauni, amewataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuweka mifumo
endelevu ya ukusanyaji na utunzaji wa taka, kudhibiti uchafuzi wa mazingira na
kuchukua hatua za kupunguza athari za mvua za El Niño.

Waziri Masauni amesema usafi wa jiji haupaswi kutegemea maagizo kutoka kwa
viongozi wa juu, bali unapaswa kuwa sehemu ya utendaji wa kila siku wa taasisi na
mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira.
Amesema Dar es Salaam ni sura ya nchi, hivyo viongozi katika ngazi zote wana wajibu
wa kuhakikisha jiji linakuwa safi na mazingira yanatunzwa wakati wote.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo jana Oktoba 11,2026 wakati wa ziara ya kutembelea na
kukagua shughuli za usafi na hatua zinazochukuliwa kutunza mazingira katika Mto
Ng’ombe, uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa licha ya changamoto za upangaji wa makazi katika baadhi ya maeneo
ya jiji, ni muhimu kuimarisha udhibiti wa utupaji holela wa taka na kuweka mifumo
madhubuti ya ukusanyaji wake ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.

Masauni amesema Ofisi ya Makamu wa Rais haitakubali kuona utekelezaji wa
shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira ukisuasua, akizitaka taasisi, halmashauri
pamoja na viongozi wa wilaya na mkoa kusimamia jukumu hilo kwa umakini na
uwajibikaji.
Ameeleza kuwa taka hazipaswi kuonekana kama uchafu pekee, bali zinaweza kuwa
chanzo cha uchumi na fursa za ajira kwa wananchi endapo zitakusanywa, kutunzwa na
kuchakatwa kwa utaratibu unaofaa.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka husika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa
taka ili kuwezesha matumizi yake yenye tija na kuongeza thamani badala ya kutupwa
ovyo na kuhatarisha afya za wananchi pamoja na mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema wilaya
hiyo inaendelea kutekeleza kampeni za kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli
za usafi na utunzaji wa mazingira.