Makonda:Viza ya pamoja AFCON 2027 inakuja

10031746261-1024x682 Makonda:Viza ya pamoja AFCON 2027 inakuja

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI imesema imechukua hatua za kurahisisha uingiaji wa wageni nchini kwa kuwezesha matumizi ya Viza ya pamoja katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kati ya Tanzania, Kenya na Uganda.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyasema hayo leo Septemba 24, 2026 jijiji Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Wizara hiyo.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha watu wanaoingia Tanzania kupata fursa ya kwenda Kenya na Uganda kutazama michezo na kurejea Tanzania bila kuwa na shida.

1003174623-1024x682 Makonda:Viza ya pamoja AFCON 2027 inakuja

Makonda amesema Serikali imeanza utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na mawaziri wa nchi hizo kuhusu namna ya kurahisisha usafiri wa watu kati ya nchi hizo.

“Kazi tunayofanya mimi na wenzetu wa vyombo vya uhamiaji chini ya wizara zetu za mambo ya ndani, ni pamoja na kurahisisha na ku-create ile free movement kati ya nchi moja kwenda nchi nyingine,” amesema.

Amesema alipata nafasi ya kwenda Nairobi na kukutana na mawaziri wenzake, ambapo walijadili namna ya kurahisisha watu kuingia katika nchi hizo wakati wa mashindano hayo.

“Nilipopata nafasi ya kwenda Nairobi kukutana na mawaziri wenzangu tulijadili ya kwamba tutafute namna ya kurahisisha mambo ili watu waweze kuingia kwenye nchi zetu bila shida,” amesema.

10031746301-1024x682 Makonda:Viza ya pamoja AFCON 2027 inakuja

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imeshatoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa mpango huo, huku Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwa imetoa taarifa na hatua husika kupelekwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.

“Tunamshukuru sana Rais kupitia kwa Waziri Mkuu kwa kutoa maelekezo ya namna ambavyo hili jambo tuliendee. Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani ameshatupa noti na sisi tumeshapeleka fomu husika kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Nje na kuhakikisha kwamba nchi yetu pia itafikika kirahisi,” amesema.

Makonda amesema moja ya maeneo yanayofanyiwa kazi ni kuoanisha mfumo wa vyombo vya uhamiaji kati ya Tanzania, Kenya na Uganda.

Amesema mfumo huo ukikamilika, mtu atakayeingia Tanzania atakuwa na uwezo wa kwenda Kenya kutazama mechi, kwenda Uganda kutazama mechi na kurejea Tanzania bila kuwa na shida.

“Hii mtu akiingia Tanzania hapa ana uwezo wa kwenda Kenya kuangalia mechi, anaweza kwenda Uganda kuangalia mechi, lakini pia ana uwezo wa kurudi kurudi hapa bila kuwa na shida yoyote,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *