
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema suala la fedha halijawa kikwazo katika maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, akieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri.
Makonda amesema hadi sasa Uwanja wa Arusha umefikia asilimia 90 ya utekelezaji, huku Uwanja wa Fumba, Zanzibar, ukifikia asilimia 85.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo, Septemba 24, 2026, Makonda amesema pia Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam unaendelea kufanyiwa maboresho makubwa, ikiwemo mabadiliko katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo na kuongeza maeneo maalumu ya skyboxes.
“Uwanja wa Arusha ni asilimia 90, Benjamin Mkapa kuna mabadiliko makubwa, tumefumua VIP na tunaongeza skyboxes, Fumba ni asilimia 85 na vifaa vipo site,” amesema Makonda.
Amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha miundombinu inayohitajika kwa ajili ya AFCON 2027 inakamilika kwa wakati.
Makonda amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa miradi hiyo zinapatikana, akisema hadi sasa maandalizi hayo hayajakwama kutokana na changamoto ya fedha.
“Mpaka sasa maandalizi hayajakwama kwa sababu ya fedha,” amesema.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoshirikiana na Kenya na Uganda kuandaa Mashindano ya AFCON 2027.