Makamu wa Rais atembelea Mount Meru, awalipia wagonjwa waliokwama

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya na kusikiliza changamoto zinazowakabili wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo.

1003228254-1024x819 Makamu wa Rais atembelea Mount Meru, awalipia wagonjwa waliokwama

Mara baada ya kuwasili hospitalini hapo, Makamu wa Rais alipokelewa na viongozi pamoja na watumishi wa hospitali hiyo, ambapo alipatiwa taarifa fupi kuhusu maendeleo, utendaji na huduma zinazotolewa.

Baada ya hapo, Ndejembi alitembelea wodi mbalimbali na kuzungumza na wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo, huku akiwapa pole kutokana na maradhi yanayowakabili na kuwafikishia salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Makamu wa Rais aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itaendelea kuipa sekta ya afya kipaumbele na kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya afya nchini.

Akiwa katika Wodi ya Wazazi, Ndejembi alieleza kufurahishwa kuwaona akina mama waliojifungua salama pamoja na watoto wao wakiwa na afya nzuri.

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi pamoja na vifo vya watoto.

10032282561-1024x819 Makamu wa Rais atembelea Mount Meru, awalipia wagonjwa waliokwama

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jitihada hizo zinaendana na dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha huduma bora na salama za afya ya uzazi zinawafikia wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na nafasi yake katika kusukuma mbele ajenda ya kupunguza vifo vya mama na mtoto barani Afrika.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais pia alipata fursa ya kuzungumza ana kwa ana na baadhi ya wagonjwa kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Wagonjwa hao walieleza kuridhishwa na huduma wanazopatiwa, huku baadhi yao wakitaja kushindwa kulipa gharama za matibabu.

1003228255-1-1024x819 Makamu wa Rais atembelea Mount Meru, awalipia wagonjwa waliokwama

Kufuatia changamoto hiyo, Makamu wa Rais aliwezesha kulipwa kwa gharama za matibabu za baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamekwama kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa, hatua iliyowapa unafuu wagonjwa hao pamoja na familia zao.

Ziara hiyo imempa Makamu wa Rais nafasi ya kujionea moja kwa moja huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Mount Meru, kusikiliza wananchi wanaozitumia na kufahamu changamoto zinazowakabili, huku akisisitiza kuendelea na hatua za kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya nchini.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais alitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, kuwasalimu wananchi na kujionea hali ya mazingira mkoani humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *