
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MRAJIS wa Vyama vya Ushirika Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Kongamano la 26 la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA Congress 2026) linatarajiwa kuwa chachu ya kuboresha usimamizi na kuongeza ufanisi katika vyama hivyo nchini.
Ndiege amesema kongamano hilo, linalofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, limewakutanisha washiriki zaidi ya 600 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha ushirika, ikiwemo matumizi ya teknolojia, takwimu na mifumo bora ya utawala.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ndiege amesema kongamano hilo lililoanza Oktoba 11 na linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 16, 2026, limekuwa na mafunzo mbalimbali yanayolenga kuwajengea uwezo viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika.
Amesema mafunzo hayo yanahusu usimamizi na utawala bora, matumizi ya teknolojia katika shughuli za vyama vya ushirika, matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi, pamoja na namna ya kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika sekta hiyo.
“Tunatarajia washiriki watakaotoka hapa na kurejea katika vyama vyao wataongeza ufanisi katika maeneo tuliyojadili, ikiwemo usimamizi, matumizi ya teknolojia na ushiriki wa wanawake na vijana,” amesema Ndiege.
Ameongeza kuwa katika mijadala ya kongamano hilo, teknolojia mpya, hususan akili unde (AI), imepewa nafasi muhimu kutokana na uwezo wake wa kusaidia kuboresha utoaji wa huduma, kuhamasisha wanachama na kuongeza ufanisi wa shughuli za vyama vya ushirika.
Kwa mujibu wa Ndiege, wataalamu kutoka ndani na nje ya Tanzania wanashiriki katika mijadala hiyo kwa lengo la kutoa mapendekezo yatakayosaidia vyama vya ushirika kutumia teknolojia zilizopo katika kuboresha utendaji wao.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha imani ya wananchi kwa vyama vya ushirika, hasa kutokana na changamoto za usimamizi zilizokuwepo hapo awali na ambazo ziliathiri uaminifu wa baadhi ya wanachama kwa taasisi hizo.“Tunategemea mkutano huu uwe chachu ya kuongeza ubora wa usimamizi katika vyama vya ushirika na kurejesha imani ya wananchi katika sekta hii,” amesema.
Aidha, Ndiege amesema Tanzania imenufaika na fursa ya kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazohusisha usafiri, malazi na huduma nyingine zinazotolewa kwa wageni, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kupata maarifa yatakayochangia maendeleo ya vyama vya ushirika.
