Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KONGAMANO la Nne la Kitaifa la Uboreshaji wa Huduma za Maktaba linatarajiwa kuanza kesho hadi Oktoba 22, mwaka huu, katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, jijini Dar es Salaam, likiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha huduma hizo kupitia mageuzi ya kidijitali kwa ajili ya kukuza maarifa na ujuzi kwa maendeleo endelevu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo litakalowakutanisha wadau wa serikali na sekta binafsi, wachapishaji, waandishi, wasomaji na washirika wa maendeleo.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, amesema kaulimbiu ya kongamano hilo imejikita katika maboresho ya huduma za maktaba kupitia mageuzi ya kidijitali, kukuza maarifa na ujuzi kwa maendeleo endelevu.
“Kaulimbiu yetu imejikita katika maboresho ya huduma za maktaba kupitia mageuzi ya kidijitali, kukuza maarifa na ujuzi kwa maendeleo endelevu,” amesema Dkt. Ruzegea wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kongamano hilo.
Amesema miongoni mwa matukio makubwa yatakayofanyika ni uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao ya Taifa (Integrated National Digital Library System), pamoja na programu tumishi itakayowawezesha wananchi kupata huduma za maktaba kupitia simu za mkononi.
Amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa machapisho na taarifa kwa kutumia teknolojia, sambamba na mwelekeo wa taifa wa kuimarisha matumizi ya kidijitali.

Hata hivyo, Dkt. Ruzegea amesema mfumo huo hautamaanisha kuwa kila kitabu kitapatikana chote mtandaoni, kwa kuwa machapisho yanayolindwa na hakimiliki yatahitaji utaratibu maalumu wa makubaliano na wenye haki hizo.
Aidha, amesema kongamano hilo litatambulisha maboresho ya sheria ya huduma za maktaba na kanuni zake, zitakazowapa wadau nafasi ya kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa huduma hizo katika mazingira ya kidijitali.
Kongamano hilo litaambatana na Tamasha la Vitabu na Usomaji, maonyesho ya machapisho na mijadala kuhusu maendeleo ya maktaba za jamii. Pia, litaadhimisha miaka 37 ya chuo cha mafunzo ya ukutubi kinachohusishwa na TLSB.