Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika

IMG-20261017-WA0003-1024x665 Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amezitaka taasisi za ushirika wa akiba na mikopo barani Afrika (SACCOS) kutekeleza maazimio ya Kongamano la 26 la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA Congress 2026) ili kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kombo amesema mafanikio ya kongamano hilo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya hotuba zilizotolewa, bali kwa matokeo halisi yanayojumuisha kuboreshwa kwa maisha ya wananchi, biashara kupata mitaji, kuongezeka kwa ajira na maendeleo ya jamii.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kongamano hilo jijini Dar es Salaam, amezitaka taasisi hizo kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji wa maazimio utakaobainisha vipaumbele, majukumu ya kila taasisi na malengo yanayopimika ili kurahisisha ufuatiliaji na tathmini ya mafanikio.

“Ujumbe wangu kwenu ni kwamba mkutano wa Dar es Salaam usikumbukwe tu kama mahali tulipokutana, bali kama mahali tulipojizatiti kuleta mabadiliko na matokeo yanayopimika,” amesema Kombo.

Amezitaka taasisi hizo kurejea katika nchi zao zikiwa na dhamira ya kuimarisha utawala bora, kuharakisha mabadiliko ya kidijitali yanayowajibika na kupanua fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuelekeza rasilimali za vyama vya ushirika katika sekta za uzalishaji, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, akieleza kuwa uwekezaji huo unaweza kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Kombo amesema vyama hivyo vinapaswa kuhakikisha vinalinda akiba na maslahi ya wanachama, huku vikiimarisha ushirikiano wa vitendo kati ya taasisi za ushirika katika mataifa ya Afrika.

Ameeleza kuwa Bara la Afrika lina rasilimali watu, vipaji na fursa nyingi za kiuchumi, lakini linahitaji taasisi imara, ushirikiano na uaminifu ili kutumia rasilimali hizo kwa manufaa ya wananchi.

“Tusilenge tu kukusanya akiba, bali tutengeneze fursa; tusilenge tu kuimarisha taasisi, bali tuboreshe maisha ya watu wetu,” amesema.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya Afrika yanahitaji zaidi ya kauli na mipango, yakihitaji uwekezaji wa rasilimali fedha na ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa zilizopo.

Kombo amehitimisha kwa kuzitaka nchi za Afrika kuendeleza mshikamano na kuweka nguvu katika utekelezaji wa maazimio ya kongamano hilo ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika bara hilo.

IMG-20261017-WA0007-1024x682 Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika
IMG-20261017-WA0004-1024x681 Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika
IMG-20261017-WA0005-1024x673 Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika
IMG-20261017-WA0001-1024x672 Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika
IMG-20261017-WA0002-1024x685 Kombo Azitaka SACCOS Afrika Kutekeleza Maazimio kwa Matokeo Yanayopimika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *