
Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
WANANCHI wanaoishi kuzunguka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro wamatakiwa kuendeleza uhifadhi na kutunza mazingira kwasababu hali hiyo imesaidia hifadhi hiyo kuwa ya pili Kitaifa kwa kuingiza mapato mengi hatua itakayochochea maendeleo kutokana na fedha zinazotokana na Utalii pamoja na uhifadhi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameyasema hayo katika mkutano wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba na wananchi wa Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro na kubainisha kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ndio inayoshika nafasi ya kwanza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni na mapato makubwa kwa ujumla.
Dkt. Kijaji amefafanua kuwa kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza Utalii na uhifadhi endelevu, sambamba na kuboresha miundombinu katika hifadhi za Taifa imepelekea Hifadhi hiyo kuingiza Sh. bilioni 364.7 katika kipindi cha kuanzia Februari 2022 hadi 2026.
Katika suala la kupambana na Wanyamapori wakali na waharibifu hususani Tembo na Tumbili, Dkt. Kijaji amewahakikishia wananchi hao kuwa wizara anayoiongoza itaendeleza jitihada za kukabiliana na madhara yanayosababishwa na Wanayamapori hao kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo teknolojia za kisasa.
Aidha, amewapongeza wananchi hao, kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika Uhifadhi Endelevu wa Hifadhi hiyo yenye vivutio adimu duniani ukiwamo Mlima wa Kilimanjaro, kwa kuwa, faida yake ni kubwa kama vile ajira hasa kwa vijana.



