Kibaha yanunua magari 7 kuboresha huduma za ukusanyaji wa mapato

WhatsApp-Image-2026-03-30-at-05.31.45-1024x682 Kibaha yanunua magari 7  kuboresha huduma za ukusanyaji wa mapato

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imenunua magari saba mapya yenye thamani ya Sh. bilioni 1 na milioni 356 kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Ununuzi wa magari hayo ulipitishwa na Baraza la Madiwani kupitia bajeti hiyo, ambapo magari hayo yanatarajiwa kutumika katika idara mbalimbali za halmashauri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi pamoja na kuimarisha shughuli za ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema ununuzi wa magari hayo ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.

Amesema kuwa magari hayo yamenunuliwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, jambo linaloonesha mafanikio katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi mzuri wa fedha za umma.

“Tunazingatia maono ya Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha tunakusanya mapato kwa ufanisi na kuyatumia kuboresha huduma kwa wananchi, lengo likiwa ni kupeleka tabasamu kwa wakazi wa Manispaa ya Kibaha,” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Ameongeza kuwa hadi sasa halmashauri imepokea magari matatu kati ya yaliyopangwa, na kufanya idadi ya magari yaliyopo kufikia saba, ambayo yote yatatumika kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya halmashauri.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ameipongeza menejimenti ya halmashauri hiyo kwa mafanikio ya ukusanyaji wa mapato, akieleza kuwa manispaa hiyo imeshika nafasi ya pili kati ya halmashauri 184 nchini.
Amesema mafanikio hayo yanaakisi utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anatamani kuona wananchi wanahudumiwa kwa haraka na changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

“Tunapaswa kuhakikisha magari haya yanatumika kama ilivyokusudiwa, hasa katika ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa wananchi ili kuongeza bajeti ya maendeleo,” amesema Dkt. Mawazo.

Naye Mkuu wa Idara ya Utumishi na Rasilimali Watu, Mrisho Mlele, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watumishi wa umma, akibainisha kuwa ununuzi wa magari hayo utasaidia kuongeza ufanisi wa kazi.
Amesema magari hayo yatawezesha ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo, kushughulikia kero za wananchi pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeeleza kuwa itaendelea kutumia mapato yake ya ndani kwa ufanisi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.

WhatsApp-Image-2026-03-30-at-05.31.43-1-1024x682 Kibaha yanunua magari 7  kuboresha huduma za ukusanyaji wa mapato
WhatsApp-Image-2026-03-30-at-05.31.43-1024x682 Kibaha yanunua magari 7  kuboresha huduma za ukusanyaji wa mapato
WhatsApp-Image-2026-03-30-at-05.31.40-1024x682 Kibaha yanunua magari 7  kuboresha huduma za ukusanyaji wa mapato
WhatsApp-Image-2026-03-30-at-05.31.37-1024x682 Kibaha yanunua magari 7  kuboresha huduma za ukusanyaji wa mapato

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *