JKT yatwaa Tuzo ya kwanza kilimo na uvivu Sabasaba

IMG-20260704-WA0000 JKT yatwaa Tuzo ya kwanza kilimo na uvivu Sabasaba


-Yajipanga kushiriki dira ya Taifa 2050

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), limeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha uzalishaji wa bidhaa bora za kilimo na uvuvi kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku likitangaza mikakati ya kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Ushindi huo unakuja kufuatia juhudi za jeshi hilo kupitia vikosi vyake na Shirika la Uzalishaji Mali la Suma JKT, katika kuzalisha bidhaa zenye tija na kutoa mafunzo ya kisasa kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maonyesho ya Sabasaba na Nane Nane Kitaifa kwa JKT, Brigedia Generali, Shija Lupi, ameeleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya ushirikiano na utekelezaji makini wa maelekezo kutoka kwa viongozi wakuu wa jeshi hilo.

“Siri kubwa ya mafanikio ya ushindi huu, kwanza, kama unavyojua sisi ni watu wa kutekeleza maelekezo.

“Maelekezo yanayotolewa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Generali, Rajabu Nduku Mabele ambaye mara nyingi amekuwa akielekeza vikosi na shirika la uzalishaji mali la Suma JKT kufanya vizuri na kuzalisha bidhaa bora,” alisema Brigadia Generali Lupi.

Brigadia Generali Lupi alibainisha kuwa JKT imekuwa mstari wa mbele (pioneer) katika sekta ya kilimo si tu kwa kulima mashamba makubwa kibiashara na kupata chakula, bali pia kwa kuwa kitovu cha mafunzo ya bure kwa Watanzania wanaotaka kuongeza tija katika uzalishaji.

“Sisi hatutozi mtu hela, ukifika pale unapewa maelekezo na unafuata. Kwa hiyo, mchango wetu uko katika nyanja hizo za sisi wenyewe kuzalisha kwa tija, kibiashara na chakula lakini vile vile tunatoa mafunzo kwa Watanzania wenzetu waweze kuzalisha,” alisisitiza.

Kuhusu ufugaji na uvuvi, alieleza kuwa jeshi hilo limejipenyeza kikamilifu kupitia kampuni ya Sumaponics inayojenga mitambo na mabwawa ya kisasa ya samaki, pamoja na uendeshaji wa ranchi kubwa za mifugo kama vile Misenyi, Oljoro, na Masinga, ambako pia ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha maziwa unaendelea.

Akizungumzia Dira ya taifa 2050, amesema mikakati yake yote ya sasa inalenga kuendana na fursa zilizoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya 2050, ikigusa maeneo ya viwanda, kilimo, na biashara za moja kwa moja.

“Tunajitahidi kufanya kila eneo kwa hakika kabisa kwamba tunaifikia lengo la 2050 kama dira ya taifa inavyosema… Tunajipanga tena sasa baada ya hapa tutaboresha zaidi bidhaa zetu ili tuendelee kuonekana na kuwa washindi kila mwaka,”alisema.

Maonesho hayo yanapoelekea ukingoni, JKT imetoa wito kwa wananchi wote kutembelea banda lao ili kujionea bidhaa za kisasa, zikiwemo samani (furniture) na bidhaa za viwandani, pamoja na kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa jeshi hilo.

IMG-20260704-WA0002 JKT yatwaa Tuzo ya kwanza kilimo na uvivu Sabasaba
IMG-20260704-WA0001-1024x746 JKT yatwaa Tuzo ya kwanza kilimo na uvivu Sabasaba

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *