JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuandaa taarifa za kina zinazojibu maswali halisi ya wananchi kuhusu gharama, upatikanaji na usalama wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, badala ya kuishia kueleza faida za nishati hiyo bila kugusa changamoto zinazowakabili watumiaji.

Wito huo umetolewa leo Novemba 13, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya waandishi wa habari Tanzania(JAB) , Wakili Patrick Kipangula, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR -PC), uliokwenda sambamba na mada ya Nishati Safi ya Kupikia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

1003737016-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

Alisema mafanikio ya ajenda hiyo hayawezi kupimwa kwa uwepo wa teknolojia pekee, bali pia uwezo wa wananchi kumudu gharama na kupata huduma hizo kwa urahisi.

Amesema familia inayotaka kuacha matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia gesi inahitaji kupata taarifa sahihi kuhusu gharama za kununua jiko na mtungi, mahali pa kupata gesi, gharama za kujaza mtungi na usalama wa vifaa hivyo.

1003737013-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

“Maswali haya yanaonesha kwamba mafanikio ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hayategemei uwepo wa teknolojia pekee, bali pia uwezo wa wananchi kumudu gharama, kupata huduma kwa urahisi na kuwa na taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi,” amesema.

Amesema hali ni hiyo hiyo kwa familia zinazotaka kutumia majiko ya umeme, ambazo zinahitaji kufahamu gharama za matumizi, upatikanaji wa vifaa vinavyofaa na uhakika wa huduma ya umeme.

IMG-20261113-WA0099-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

Kutokana na hali hiyo, amewataka waandishi kuhakikisha taarifa wanazoandaa zinazingatia mazingira halisi ya wananchi, zikiwemo familia zenye kipato cha kawaida, wafanyabiashara wadogo na wananchi wa maeneo ya vijijini wanaohitaji kufahamu namna ya kupata nishati hiyo katika maeneo yao.

“Kwa hiyo, habari tunazotoa zinapaswa kujibu maswali ya wananchi na kuwasaidia kufanya uamuzi sahihi,” amesema.

1003734216-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwapa wananchi nafasi ya kueleza uzoefu wao kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa kufanya mahojiano na familia zilizoanza kutumia nishati hiyo, wafanyabiashara wadogo, wapishi wa shule na taasisi mbalimbali ili kubaini mafanikio na changamoto wanazokutana nazo.

Amesema habari zinazojumuisha ushuhuda wa wananchi na ushahidi wa kutosha zinaweza kusaidia Serikali na wadau wengine kutambua maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika utekelezaji wa ajenda hiyo.

1003737004-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

Wakili Kipangula pia amewataka wahariri na waandishi wa habari kuzingatia takwimu sahihi, ukweli na maadili ya taaluma, akisisitiza kuwa kasi ya kusambaza taarifa kupitia vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali haipaswi kuwa sababu ya kutoa habari ambazo hazijathibitishwa.

“Tunapaswa kukumbuka kwamba habari ya kwanza si bora kama si sahihi. Mwandishi wa habari mwenye weledi si yule anayewahi kutoa taarifa pekee, bali ni yule anayehakikisha kwamba taarifa anayotoa ni ya kweli, imehakikiwa na ina manufaa kwa jamii,” amesema.

1003737005-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

Kwa mujibu wa Kipangula, Serikali imeweka Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kufikisha matumizi ya nishati hiyo kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.

Amesema mkakati huo ni sehemu muhimu ya safari ya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akibainisha kuwa mafanikio yake yanahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za kitaalamu na vyombo vya habari.

1003737014-1-1024x683 JAB yahamasisha habari zenye majibu ya changamoto za nishati safi ya kupikia

Ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi yana mchango katika kulinda afya za wananchi, kupunguza muda unaotumika kutafuta kuni, kuhifadhi mazingira na kufungua fursa mpya za kiuchumi kupitia biashara ya vifaa, usambazaji wa nishati, huduma za ufundi, teknolojia na ubunifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *