
Na Mwandishi Wetu, Iringa
Timu ya mpira wa kikapu ya wavulana kutoka Mkoa wa Dar es Salaam imefanikiwa kutetea ubingwa wake baada ya kuibuka mabingwa wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) 2026 yanayofanyika mkoani Iringa.
Dar es Salaam ilitwaa taji hilo baada ya kuichapa timu ya Mkoa wa Rukwa kwa vikapu 52–41 katika mchezo wa fainali uliochezwa Juni 16, 2026 kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Lugalo, Manispaa ya Iringa.
Ushindi huo umeifanya Dar es Salaam kuendelea kudhihirisha ubora wake katika mchezo wa kikapu kwa kutetea taji ililolishinda mwaka uliopita, huku ikihitimisha mashindano ya kikapu wavulana kwa mafanikio makubwa.
Katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, timu ya Zanzibar ilifanikiwa kutwaa nafasi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa vikapu 45–38 dhidi ya Mkoa wa Kigoma katika mchezo uliokuwa wa ushindani mkubwa na kusisimua mashabiki waliojitokeza kushuhudia pambano hilo.
Mashindano ya UMITASHUMTA 2026 yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi Juni 17, 2026, ambapo washindi wa michezo na taaluma mbalimbali watatunukiwa kabla ya kufungwa kwa mashindano hayo yanayofanyika mkoani Iringa kwa mara ya pili mfululizo.


