COSTECH kuibuka na ubunifu wa kitaifa kilele cha miaka 40

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAADHIMISHO ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), yameibua bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, zikiwemo za afya, ufugaji wa samaki na upatikanaji wa nishati(Gesi).

Miongoni mwa bunifu hizo ni Mkanda wa Salama unaolenga kumsaidia mama anayepata tatizo la kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua, chanjo ya samaki pamoja na teknolojia ya kuzalisha nishati(gesi) kwa kutumia maji.

1003706599-1024x682 COSTECH kuibuka na ubunifu wa kitaifa kilele cha miaka 40

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema baadhi ya bunifu hizo tayari zimeanza kuingia katika hatua za uzalishaji, huku nyingine zikiendelea kufanyiwa tathmini ya usalama na uwezekano wa kibiashara.

Amesema Mkanda wa Salama ni miongoni mwa bunifu zilizooneshwa katika maonesho yaliyofanyika kwenye viunga vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo unasaidia kupunguza damu inayotoka kwa wingi kwa mama baada ya kujifungua ili kumwezesha kuwahi kupata matibabu.

“Tayari kiwanda kimefunguliwa Kimara Suka jijini Dar es Salaam na tayari hata nchi za nje kama Rwanda na nchi zingine wanaonesha kusudio la kuja kufanya manunuzi ya mkanda ule,” amesema.

1003706616-1024x682 COSTECH kuibuka na ubunifu wa kitaifa kilele cha miaka 40

Ametaja ubunifu mwingine kuwa ni chanjo ya samaki, inayolenga kukabiliana na magonjwa yanayosababisha vifo vya samaki hasa vifaranga, hususan wanaofugwa kwenye mabwawa, akidai tayari imekubalika hata na mamlaka za nchi za nje.

Pia, amesema kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, kuna mbunifu amebuni teknolojia ya kutenganisha maji na kupata gesi ya hydrogen na oxygen, ambazo kwa mujibu wa maelezo ya mbunifu huyo zinaweza kutumika katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kupikia na kusaidia huduma za hospitali.

Hata hivyo, Prof Mkenda amesema Serikali imeagiza vyombo husika kuchunguza usalama wa teknolojia hiyo na uwezekano wake wa kiuchumi ili kubaini kama inaweza kutumika kwa gharama nafuu ikilinganishwa na kuagiza gesi kutoka nje ya nchi.

Prof. Mkenda amesema maadhimisho hayo yaliyozinduliwa Julai 2 mwaka huu, yamehusisha shughuli mbalimbali, zikiwemo kliniki ya ubunifu wakati wa maonesho, maonesho ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika viunga vya Bunge pamoja na tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya tume na mikakati ya kuendeleza ajenda ya 2050 kupitia sayansi na teknolojia.

Akizungumzia umuhimu wa kuendeleza sayansi na teknolojia, Prof. Mkenda amesema maendeleo endelevu ya nchi yanategemea uwezo wa kutumia maarifa na teknolojia kuzalisha na kutatua changamoto zake yenyewe, badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje katika kila hatua.

1003706601-1024x682 COSTECH kuibuka na ubunifu wa kitaifa kilele cha miaka 40

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu ya sayansi kupitia ujenzi wa shule za sayansi kwa wasichana katika kila Mkoa, utoaji wa ufadhili wa masomo na tuzo kwa wahadhiri na vyuo vikuu vinavyofanya tafiti zinazotambulika kimataifa.

Amesema maadhimisho hayo yatahitimishwa Novemba 18 mwaka huu katika viwanja vya Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Ameeleza kuwa maonesho yataanza Novemba 17 na kuendelea Novemba 18, huku akiwataka Watanzania na wadau mbalimbali kujitokeza kushuhudia bunifu na teknolojia zitakazooneshwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *