
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatarajia kutumia Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) unaofanyika jijini Dar es Salaam, kuimarisha fursa za uwekezaji katika Uchumi wa Buluu, ikiwemo uvuvi endelevu, utalii wa baharini, kilimo cha mwani, bioeconomy na huduma za ikolojia.
Mkutano huo unaofanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), unatarajiwa pia kuunganisha Tanzania na mifuko ya kimataifa pamoja na taasisi za fedha kwa ajili ya miradi ya uhifadhi wa bahari na pwani, mabadiliko ya tabianchi, udhibiti wa uchafuzi na bioanuai.

Akizungumza kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa COP12, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amesema mkutano huo unatarajiwa kuleta fursa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, ikiwemo kuvutia uwekezaji katika Uchumi wa Buluu.
Amesema fursa hizo zitahusisha kuwaunganisha wawekezaji na maeneo ya uwekezaji katika uvuvi, utalii wa baharini, kilimo cha mwani, bioeconomy na huduma za ikolojia, sambamba na kuchochea upatikanaji wa fedha za mazingira na tabianchi.
Kwa mujibu wa Waziri Masauni, COP12 pia itatoa fursa ya kupata utaalamu, teknolojia na ushirikiano wa kikanda katika kupanga matumizi endelevu ya maeneo ya bahari kupitia utekelezaji wa Marine Spatial Planning (MSP).

Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu ya kitaifa isemayo ‘Kuelekea Uchumi wa Buluu Endelevu katika Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi kwa Manufaa ya Watu na Mazingira ya Asili: Safari ya Miaka 40.’
Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika COP12 ni kudhibiti uchafuzi wa bahari na pwani, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira ya bahari, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ustahimilivu wa jamii, miundombinu na mifumo ya ikolojia ya pwani.
Mkutano huo pia utajadili uhifadhi wa bioanuai ya bahari na pwani, ikiwemo mikoko, matumbawe, nyasi bahari na maeneo muhimu ya ikolojia, pamoja na kuendeleza Uchumi wa Buluu endelevu kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na uwekezaji, biashara, ajira na maendeleo ya jamii za pwani.
Waziri Masauni amesema Tanzania kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa COP12 kuna matarajio ya kuimarisha diplomasia ya mazingira ya Tanzania na kuongeza ushawishi wake katika masuala ya mazingira ya bahari na pwani katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Aidha, mkutano huo unatarajiwa kutoa Azimio la Dar es Salaam, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika Uchumi wa Buluu ili kuongeza fursa za uvuvi endelevu, aquaculture, utalii wa baharini, usafiri wa majini na uwekezaji unaozingatia mazingira.
Kwa upande wa jamii, Serikali inalenga kuhakikisha fursa za Uchumi wa Buluu zinawafikia wananchi, hususan jamii zinazotegemea bahari na pwani. Manufaa yanayotajwa ni pamoja na ajira, uvuvi endelevu, ufugaji viumbe maji, utalii, biashara, huduma na kuongeza thamani ya mazao.
Kupitia utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi, jamii zinazotegemea rasilimali za bahari na pwani zimepata manufaa mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa uelewa kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani na kuimarika kwa shughuli za kujipatia kipato na maisha ya jamii za wavuvi.
Manufaa hayo pia yamehusisha kushirikishwa kwa jamii katika urejeshaji na uhifadhi wa misitu ya mikoko, ikiwemo katika Delta ya Rufiji, pamoja na kuimarika kwa mazingira ya bahari na pwani kutokana na kupunguza uchafuzi kupitia miradi ya usimamizi wa taka za plastiki, maji machafu na vyanzo vingine vya uchafuzi vinavyoingia baharini.
Aidha, kupitia Uchumi wa Buluu, wananchi wa jamii za pwani wananufaika kwa kulindwa na kurejeshwa kwa mifumo muhimu ya ikolojia, ikiwemo mikoko, matumbawe na nyasi bahari, ambayo ni muhimu kwa uvuvi, kinga ya fukwe na ustawi wa jamii.
Pia, hatua hizo zinalenga kupunguza athari za mmomonyoko wa fukwe na uharibifu wa maeneo ya pwani, huku zikiongeza fursa za wananchi kushiriki katika Uchumi wa Buluu kutokana na kuimarishwa kwa usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na pwani.
Waziri Masauni amesema matarajio ya Tanzania ni kuhakikisha COP12 inaleta matokeo yanayolinda mazingira ya bahari na pwani, kuimarisha Uchumi wa Buluu, kuongeza ushirikiano wa kikanda na kimataifa na hatimaye kuleta manufaa kwa wananchi, hususan jamii zinazotegemea rasilimali za bahari na pwani.