
Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP), Jeremiah Yoram Katungu, amewataka viongozi na watendaji wa Jeshi la Magereza kuweka mbele maslahi ya taifa na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kufikia malengo ya Jeshi la Magereza.
CGP Katungu ameyasema hayo leo Novemba 6, 2026, wakati akizungumza katika kikao kazi maalum kilichowakutanisha viongozi wa Division ya Utawala na Rasilimali Watu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, CGP Katungu amesisitiza umuhimu wa wakuu wa vitengo kuweka malengo yanayopimika na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kuboresha utendaji kazi ambapo mafanikio ya Jeshi la Magereza yanategemea sana uimarishwaji wa mahusiano mazuri baina ya division moja na nyingine.
Katika hatua nyingine, CGP Katungu ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliunga mkono Jeshi la Magereza kwa kuwapandisha vyeo maafisa wa ngazi za juu 37, wakiwemo Manaibu Kamishna (DCP) 17 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi (SACP) 22.
Kwa upande wake, Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Magereza (CP), Ahmad Said Mwen-Dadi, amemshukuru Mkuu wa Jeshi kwa maelekezo yake na kuahidi kuyasimamia kikamilifu ili kuleta mabadiliko chanya ndani ya Divisheni hiyo.
Vikao vya namna hii vimekuwa ni utaratibu wa kawaida wa Mkuu wa Jeshi la Magereza, vikiwa na lengo la kukumbushana wajibu na kuhakikisha majukumu yote ya kiulinzi na kurekebisha tabia yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria.






