Mapato ya ndani yachochea ujenzi wa Barabara Ilala, bil. 14/- zatengwa

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

UWEZO wa kukusanya mapato ya ndani umeendelea kuipa nguvu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutekeleza miradi ya miundombinu, baada ya kutenga zaidi ya Shilingi bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ilala.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema hatua hiyo inaakisi maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza utegemezi wa mapato ya ndani katika kugharamia miradi ya maendeleo badala ya kutegemea wafadhili.

2-8-1024x683 Mapato ya ndani yachochea ujenzi wa Barabara Ilala, bil. 14/- zatengwa

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa mita 400, Mpogolo amesema ukuaji wa makusanyo ya Halmashauri unaipa fursa ya kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya barabara.

“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tayari imeshatenga zaidi ya Shilingi bilioni 14 kwa ajili ya miundombinu ya barabara. Tunaiomba Serikali kuona namna ya kuruhusu kiwango cha fedha zinazotengwa kufikia asilimia 15 ya mapato ya ndani ili tuweze kuwa na zaidi ya Shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara,” amesema.

Amesema fedha hizo zitasaidia kujenga barabara za lami na zege, kuboresha barabara za changarawe na kuhakikisha miundombinu iliyopo inatunzwa kwa wakati ili kuendelea kuhudumia wananchi kwa ufanisi.

3-7-1024x682 Mapato ya ndani yachochea ujenzi wa Barabara Ilala, bil. 14/- zatengwa

“Barabara hizi zinajengwa kwa gharama kubwa, hivyo ni muhimu kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuzitunza. Tukifikia asilimia 15, tutakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara,” amesema.

Mpogolo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini, akisema hatua hiyo imekuwa kichocheo cha kuharakisha utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi.

Pia ameipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI chini ya Waziri Prof. Riziki Shemdoe pamoja na viongozi wengine kwa usimamizi wa miradi ya maendeleo, huku akibainisha kuwa mafanikio yanayopatikana Ilala yanatokana na mshikamano wa viongozi na dhamira ya kuwatumikia wananchi.

4-7-1024x682 Mapato ya ndani yachochea ujenzi wa Barabara Ilala, bil. 14/- zatengwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *