NBC yakabidhi gari mshindi wa kampeni ya huduma za kidigitali

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi zawadi kuu za kampeni yake ya “Ukigusa Tu, iMOOO” kwa washindi wakubwa watatu wa kampeni hiyo ikiwamo zawadi kubwa ya gari aina Nissan X trail iliyokabidhiwa kwa Salah Ahmed Mohamed mkazi wa jijini Dar es Salaam alieibuka mshindi wa zawadi kuu ya kampeni iliyolenga kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia uchocheaji wa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali.

Hafla ya makabidhiano ya zawadi hiyo iliyohusisha pia makabidhiano ya zawadi kwa mshindi wa pili na watatu wa kampeni hiyo waliojishindia zawadi za simu janja  aina ya Iphone 17 Pro na jiko la gesi na umeme imefanyika leo Februari 26, kwenye tawi la benki ya NBC tawi la Mlimani City, jijini Dar es salaam ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja Binafsi (wadogo na wakubwa) wa benki  hiyo, Elibariki Masuke pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Masuke amesema pamoja na kutoa zawadi pia kampeni hiyo ilibeba dhamira pana ya kijamii ya kuongeza uelewa na matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali kwa makundi mbalimbali ya jamii.

Ameeleza kuwa walengwa wa kampeni hiyo walijumuisha wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wanafunzi, pamoja na wateja binafsi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kupunguza changamoto za miamala ya ana kwa ana.

Ameongeza kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa zawadi za kila wiki kwa washindi wengine wengi, zikiwamo fedha taslimu na kompyuta mpakato, kama sehemu ya kuhamasisha tabia ya kuweka akiba, kufanya miamala salama na kutumia teknolojia kwa maendeleo binafsi na ya biashara.

Naye Mkuu wa Idara ya Miamala wa NBC, Mangire Kibanda, amesema kupitia kampeni hiyo, NBC imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuchangia ajenda ya kitaifa ya ujumuishaji wa kifedha na ujenzi wa jamii inayotumia teknolojia kwa maendeleo.

“Benki tutaendelea kubuni programu na kampeni zenye kugusa maisha ya Watanzania, kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.’’ ameongeza

Akizungumza kwa niaba ya washindi wote wa kampeni hiyo, Diana Bernard, ameishukuru NBC kwa kuandaa kampeni yenye tija kwa wateja na jamii kwa ujumla. Alisema wao kama familia wamekuwa wateja wa muda mrefu wa benki hiyo kutokana na ubora wa huduma na urahisi wa matumizi ya mifumo ya kidigitali.

Mbali na zawadi ya gari, washindi wengine waliokabidhiwa zawadi zao ni Vidya Sagar, aliyejishindia simu janja aina ya iPhone 17 Pro pamoja na Beatrice Chengula wa Temeke aliyejishindia jiko la gesi na umeme.

GARI-1-1024x684 NBC yakabidhi gari mshindi wa kampeni ya huduma za kidigitali

Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Binafsi (wadogo na wakubwa) wa benki ya NBC Elibariki Masuke (kushoto) akimshuhudia, Diana Bernard ambaye ni mwakilishi  wa  Salah Ahmed Mohamed mkazi wa jijini Dar es Salaam alieibuka mshindi wa zawadi kuu ya kampeni ya “Ukigusa Tu, iMOOO” ya benki hiyo iliyolenga kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia uchocheaji wa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali. Hafla ya makabidhiano ya zawadi hiyo imefanyika jana, kwenye Tawi la Benki ya NBC Tawi la Mlimani City, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam (Picha: Mpigapicha Wetu)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *