Na Badrudin Yahaya
KIUNGO wa timu ya Simba SC, Clatous Chama, ameibuka shujaa kwa upande wa timu yake baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika za lala salama na kuiwezesha kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ulikuwa na mvutano mkali na hadi zinafika dakika za mwishoni alama tatu zilionekana kuelekea Chamazi.
Chama alifunga bao hilo kwa mpira wa adhabu ndogo alioupiga na kuingia moja kwa moja golini mara baada ya walinzi wa Azam kushindwa kuokoa.
Kabla ya bao hilo, Simba walicheza muda mwingi wakiwa nyuma kwa bao moja ambalo lilifungwa tangu dakika ya 14 kipindi cha kwanza na mshambuliaji, Prince Dude.
Bao alilofunga Dube kwenye mchezo wa leo linaendeleza rekodi yake nzuri ya kuifunga Simba kila wanapokutana katika mechi mbalimbali.
Kwa matokeo hayo, Azam wanasalia nafasi ya pili wakifikisha alama 32 ambazo ni tano nyuma ya Yanga yenye alama 37.
Kwa Simba matokeo haya yanawanyima fursa ya kuendelea kukusanya alama tatu kama walivyofanya katika mechi mbili zilizopita.
Katika msimamo wa ligi, Simba inasalia nafasi ya tatu wakifikisha alama 30 ambazo ni saba nyuma ya vinara Yanga lakini Simba wana mchezo mmoja mkononi ambao watacheza Februari 12 dhidi ya Geita Gold.