Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Simba SC, imetangaza kukamilisha usajili wa kiungo Babacar Sarr raia wa Senegal.
Kiungo huyo amejiunga Simba kama mchezaji huru mara baada ya kumaliza mkataba wake na Klabu ya US Monastir ya Tunisia mwishoni mwa mwaka jana.
Huo unakuwa ni usajili wa wa pili wa Simba kwenye dirisha hili chini ya Kocha, Abdelhak Benchikha.
Sarr aliwahi kucheza dhidi ya Cristiano Ronaldo wa Al Nassr katika mechi za michuano ya Klabu Bingwa ya Nchi za Kiarabu iliyopigwa Julai 31, mwaka jana wakati akiichezea Monastir iliyocheza na Yanga msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mechi hiyo, Al Nassr ilishinda mabao 4-1 na ndio iliyobeba taji ikiifunga Al Hilal.
Kiungo huyo mkabaji anayetumia zaidi mguu wa kulia, ana miaka 26 na ana uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.
Mchezaji wa kwanza kusajiliwa alikuwa ni Saleh Karabaka ambaye alijiunga na Simba akitokea JKU.
Mbali na wachezaji hao lakini pia Simba inatajwa kumalizana na Ladack Chasambi wa Mtibwa Sugar na Edwin Balua wa Tanzania Prison.
Pia Simba inamfanyia majaribio kiungo mshambuliaji raia wa Zimbabwe, Michael Charamba ambaye alicheza mchezo wa Kombe la Mapinduzi baina ya Simba dhidi ya APR.