Kanuni yaitoa Simba SC AFL ikitoka sare 1-1 na Al Ahly

Na Badrudin Yahaya

NI! Kanuni tu! Ndivyo mashabiki wa timu ya Simba SC watakavyokuwa wakitamba katika mitaa mbalimbali nchini baada ya kuishuhudia timu yao ikitoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly ugenini katika michuano ya AFL na kutolewa mashindano kwa bao la ugenini.

Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, nchini Misri, umeifanya Al Ahly kutinga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya timu hizo kufungana jumla ya mabao 3-3.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Kocha wa Simba kwenye mchezo huo alianza kwa kuwapa heshima wapinzani wake na kuwaachia wabaki na mpira kwa muda mwingi lakini bila kuwa na madhara kwenye lango lao.

Mshangao pengine kwa mashabiki wengi wa soka nchini, ilikuwa ni kuanzishwa kikosini kwa nahodha mkongwe wa Simba, John Bocco ambaye alikuwa akiongoza safu ya ushambuliaji akisaidiwa na Kibu Denis na Saido Ntibanzokiza.

Wenyeji Al Ahly walijaribu kutengeneza nafasi nyingi lakini kikwazo ilikuwa ni safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa inaongozwa na Henock Inonga na Che Malone Fondoh waliokuwa imara kuondoa mauzauza yote yaliyoelekezwa langoni mwao.

Hadi mwamuzi Jean Ndala anapuliza kipyenga cha kutamatisha dakika 45 za kwanza timu hizo zilikuwa suluhu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’, kufanya mabadiliko ya kumtoa Bocco na nafasi yake kuchukuliwa na Jean Baleke.

Mabadiliko hayo yaliwaongezea Simba nguvu kwenye safu ya ushambuliaji na kuanza kutengeneza nafasi ambazo baada ya muda zilizaa matunda.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kuandika bao kwenye mchezo huo kupitia Sadio Kanoute kwenye dakika ya 68 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira uliotoka kwa Ntibazonkiza, hata hivyo, Mahmoud Kahraba alisawazishia timu yake dakika chache baadaye.

Kiungo mshambuliaji wa Al Ahly, Percy Tau alijikuta akipoteza nafasi nyingi nzuri za kufunga kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza kwa kukosa umakini anapolikaribia goli.

Simba sasa wanarudi nyumbani wakiwa wamejihakikishia kitita cha dola milioni 1 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *