LATRA CCC yataka matumizi ya tiketi za kielekroniki kuepuka utapeli

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BARAZA la Watumiaji Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) limewataka wananchi wanaotumia usafiri wa ardhini kutumia tiketi za kielektroniki wanapopanga safari zao, ili kujilinda dhidi ya udanganyifu na utapeli, hususan katika kipindi cha kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Akizungumza katika maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Usafiri Endelevu Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa LATRA CCC, Daudi Daudi, amesema matumizi ya tiketi hizo yanasaidia kupunguza udanganyifu unaofanywa na watu wanaouza tiketi zisizo na uthibitisho.

1003909005-1024x1018 LATRA CCC yataka matumizi ya tiketi za kielekroniki kuepuka utapeli

Amesema baraza hilo limeshiriki maadhimisho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu kuhusu haki na wajibu wao pamoja na taarifa sahihi zinazohusu huduma za usafiri wa ardhini, akibainisha kuwa elimu kwa watumiaji ni sehemu muhimu ya kuhakikisha sekta hiyo inakuwa salama kwa maslahi ya abiria.

Daudi amesema maadhimisho hayo yanayofanyika Novemba 26 kila mwaka yanaongozwa na kaulimbiu inayohimiza kuharakisha usafiri endelevu ulio salama, rafiki kwa mazingira na shirikishi kwa makundi yote ya jamii, hivyo kutoa fursa kwa wadau kujadili namna ya kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji.

Amesema katika siku tatu za maonesho hayo, banda la LATRA CCC lilipokea takribani watu 200 waliotembelea kupata elimu kuhusu huduma za usafiri, huku maafisa wa baraza hilo wakiendelea kutoa ufafanuzi na kushiriki mijadala mbalimbali iliyohusisha wadau wa sekta hiyo.

1003909004-1024x1023 LATRA CCC yataka matumizi ya tiketi za kielekroniki kuepuka utapeli

Ameongeza kuwa baraza linaendelea na mikakati ya kuwafikia wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia kamati za watumiaji huduma za usafiri za mikoa (RCC), vyombo vya habari, redio, televisheni na majukwaa ya kidijitali ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za usafiri.

Akizungumzia maandalizi ya safari za Desemba, Daudi amewataka abiria na watoa huduma za usafiri kupanga safari zao mapema kutokana na ongezeko la mahitaji ya usafiri katika kipindi hicho.

Amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya abiria kudanganywa na watu wanaojitokeza katika vituo vya mabasi, hususan stendi, kwa kujifanya kuwa na uwezo wa kuwasaidia kupata tiketi, hali inayoweza kusababisha wananchi kulipia huduma ambazo hawana uhakika nazo.

Amefafanua kuwa abiria hawahitaji kufika katika vituo vya mabasi ili kupata tiketi za kielektroniki, bali wanaweza kuzikata wakiwa nyumbani au mahali popote walipo kwa kutumia simu janja, kompyuta mpakato au kompyuta nyingine yenye huduma ya intaneti.

1003909055 LATRA CCC yataka matumizi ya tiketi za kielekroniki kuepuka utapeli

“Mwananchi anaweza kupata huduma hiyo kwa kuingia katika tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), ambayo ni www.latra.go.tz, na kufuata kiunganishi kinachomwelekeza kwenye mfumo wa tiketi za kielektroniki unaounganisha watoa huduma mbalimbali za usafiri,” amesema.

Ameongeza kuwa mfumo huo umeunganisha huduma za ukataji tiketi kwa usafiri wa mabasi na reli, hivyo kumpa mwananchi fursa ya kupata huduma kupitia sehemu moja badala ya kutafuta mifumo tofauti kwa kila kampuni ya usafiri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa LATRA CCC, Fatuma Kulita, amewahimiza watumiaji wa huduma za usafiri ardhini kukata tiketi za safari zao mapema kupitia mifumo ya mtandao ili kuepuka usumbufu wakati wa kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Amesema kipindi hicho huwa na ongezeko kubwa la wasafiri, hivyo maandalizi ya mapema yatasaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi na kuepuka changamoto, ikiwemo utapeli wa fedha unaofanywa na watu wasio waaminifu.

Fatuma amesema LATRA CCC imeshiriki maadhimisho hayo kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za usafiri kuhusu haki na wajibu wao wanapotumia vyombo vya usafiri ardhini.

“Matumizi ya mifumo rasmi ya mtandao katika ununuzi wa tiketi ni hatua muhimu ya kujilinda dhidi ya matapeli na kuhakikisha safari zinafanyika kwa utaratibu unaostahili,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *