
Rais Samia Suluhu Hassan, amemwelekeza Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, kuunda timu ya wahandisi itakayopitia upya makisio ya gharama za ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ili kubaini uhalisia wake na kuharakisha kuanza kwa kazi hiyo.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Novemba 27, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule, akimtaka pia Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Mitawi, kushirikiana na Waziri wake, Paul Makonda, kuhakikisha changamoto zinazoikabili sekta hiyo zinapatiwa ufumbuzi.
Amesema amepata taarifa za mvutano uliopo kuhusu makisio ya gharama za ukarabati wa uwanja huo, baada ya mshauri elekezi kubaini kuwa bajeti iliyopendekezwa ni kubwa kuliko inavyopaswa, hali iliyosababisha kutokuwepo kwa mwafaka na kuchelewesha kuanza kwa kazi.
“Katibu Mkuu Kiongozi, lifuatilie hilo, tengeneza timu ya wahandisi waangalie hiyo bajeti kama iko sawa kazi iendelee, kama haiko sawa irekebishwe,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa kuchelewa kwa ukarabati huo kunatia wasiwasi, hasa ikizingatiwa kuwa muda wa maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) unazidi kusogea, huku Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa miongoni mwa miundombinu muhimu inayohitaji maandalizi.
Amesisitiza kuwa mapitio ya gharama yafanyike kwa haraka ili kubaini makisio sahihi na kuwezesha ukarabati kuanza bila kuchelewa zaidi.
