
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimesaini mikataba mitatu ya mikopo nafuu yenye thamani ya euro milioni 175, sawa na shilingi bilioni 513, kwa ajili ya kufadhili miradi ya maji na usafi wa mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, kuboresha miundombinu ya chakula katika miji ya Mwanza na Tanga, pamoja na kuendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji wadogo.
Mikataba hiyo imesainiwa Jijini Paris na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa AFD, Christophe Lecourtier ambapo Mikopo hiyo inajumuisha Euro Milioni 90 (shilingi bilioni 263.8) kwa ajili ya Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika maeneo ya Ziwa Victoria (LV WATSAN II), Euro Milioni 55 (shilingi bilioni 161.2) kwa Programu ya Uwekezaji Endelevu katika Mifumo ya Chakula Mijini (TASUFIP), na euro milioni 30 (shilingi bilioni
87.9) kwa Programu ya Kuendeleza Ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa kwa Wafugaji Wadogo kwa Kuzingatia Mabadiliko ya
Tabianchi (C-SDTP).
Miradi hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira, kuimarisha miundombinu ya biashara na usambazaji wa chakula katika miji ya Mwanza na Tanga, pamoja na kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuwawezesha wafugaji wadogo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, miradi ya maji na mifumo ya chakula pia itanufaika na ruzuku ya nyongeza kutoka Umoja wa Ulaya kupitia AFD, huku programu ya ufugaji ikifadhiliwa kwa pamoja
na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Aidha, akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo,Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema mafanikio ya mikataba hiyo yataonekana kupitia utekelezaji wa miradi itakayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja ambapo Alibainisha kuwa ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na AFD sasa umefikia Euro Bilioni 1.3, sawa na Sh. Trilioni 3.81.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania chini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Asha Khamis Abdulla, na Kamishna wa Fedha za Nje, Rished Bade.


