Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA imepata ahadi za kifedha na fursa za uwekezaji zenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 4.7 kupitia Mkutano wa 31 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), zikiwemo fedha za nishati safi ya kupikia, uhifadhi wa mazingira, nishati jadidifu na miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ahadi hizo zilizotolewa na taasisi za kimataifa, washirika wa maendeleo na nchi mbalimbali zinatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimazingira nchini, kuimarisha matumizi ya nishati safi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa taarifa ya matokeo na manufaa ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo uliofanyika Antalya, nchini Uturuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni amesema ushiriki wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha nchi kupata mafanikio makubwa na kuendeleza vipaumbele vyake katika ajenda ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema miongoni mwa ahadi hizo ni Dola milioni 54 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kununua majiko 70,000 ya kisasa yanayotumia umeme kwa shule na vituo vya afya. Benki hiyo pia imeahidi Dola milioni 26 kwa ajili ya mradi wa kuhifadhi mifumo ikolojia ya pwani na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.

Aidha, amesema Serikali ya Uingereza kupitia UK Aid imeahidi Pauni milioni mbili kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na Pauni milioni mbili nyingine kwa nishati jadidifu, huku ikisaidia wananchi milioni moja kupata majiko ya umeme kwa utaratibu wa kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia bili za umeme.
“Tasisi ya SEforALL imeahidi kuijumuisha Tanzania katika nchi zitakazonufaika na uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni nne kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, sambamba na kusaidia nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa majiko na teknolojia zinazohusiana na nishati hiyo.

“Pia, kampuni ya UpEnergy imeahidi kuendeleza mradi wa nishati safi ya kupikia katika shule 3,000 za umma wenye thamani ya takribani Dola milioni 30 kupitia ushirikiano wa Tanzania na Japan katika biashara ya kaboni,”amesema.
Wakati huo huo, amesema Saudi Arabia imeahidi kuendelea kufadhili miradi ya nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia pamoja na kuunga mkono matumizi ya gesi asilia kama nishati ya mpito.

Alisema, miongoni mwa mafanikio mengine ni ahadi ya Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuidhinisha miradi yenye thamani ya Dola milioni 40 kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), huku Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Kijani (GCF) ukiahidi Dola milioni sita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa Tanzania kuandaa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu umeidhinisha mchakato wa kupata Dola milioni 20 kupitia CRDB Bank kwa ajili ya mradi wa kusaidia jamii za visiwa vidogo, maeneo ya pwani na kanda za maziwa, hususan Pemba, Unguja, Kigoma na Pwani. Vilevile, International Solar Alliance imeiweka Tanzania katika mpango wa Dola milioni 200, huku U.S.-China Green Fund ikiwa imeijumuisha katika mpango wa Dola milioni 300 wa kusaidia nchi zinazoendelea katika eneo la nishati safi ya kupikia.

Mhandisi Masauni amesema mafanikio hayo yanakwenda sambamba na hatua za kuimarisha uwezo wa Tanzania kunufaika na fedha za kimataifa, akieleza kuwa GCF imetoa ithibati kwa NEMC, na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zenye taasisi mbili zilizoidhinishwa kupata fedha za mfuko huo, ambazo ni NEMC na CRDB Bank.
Katika hatua nyingine, amesema Tanzania imesaini makubaliano ya ushirikiano na Sekretarieti ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ili kuwa mwenyeji wa mikutano ya tabianchi, ikiwa ni nchi ya pili duniani kufanya hivyo.

“Kupitia makubaliano hayo, nchi inajiandaa kuwa mwenyeji wa mikutano miwili ya UNFCCC kuanzia Februari 2027, hatua inayotarajiwa kuimarisha diplomasia ya tabianchi na kukuza utalii wa mikutano,”amesema.
Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) imesaini mikataba ya ushirikiano na taasisi za kimataifa za IETA, Evercity UG na Verra kwa ajili ya kujenga uwezo, kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni, usajili na uthibitishaji wa miradi pamoja na upatikanaji wa viwango vya kaboni vinavyokidhi viwango vya kimataifa.

Masauni amesema mafanikio mengine ni Tanzania kupata uthibitisho wa kuwa mwenyeji na kuanzisha Kituo cha Vijana Wajadili wa Tabianchi Afrika (Youth Negotiators Centre), kitakachojenga uwezo wa vijana kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Pia, Zanzibar imetunukiwa cheti cha kutambuliwa kama Jiji Linalosimamia Taka Vizuri (Zero Waste City) na kuchaguliwa kuwa miongoni mwa maeneo 20 ya awali katika nchi 11 duniani yatakayotekeleza Mpango wa Kimataifa wa Maeneo Yasiyo na Taka.
Akifafanua kuhusu utekelezaji wa ahadi hizo, Masauni amesema Serikali itafuatilia kwa karibu ahadi za kifedha na fursa za uwekezaji zilizopatikana ili kuhakikisha rasilimali hizo zinafika nchini na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Jukumu letu sasa ni kuhakikisha kuwa ahadi na fursa hizi zinafuatiliwa kwa karibu, taratibu zinakamilishwa na rasilimali zinageuzwa kuwa miradi na manufaa halisi kwa wananchi,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa matokeo ya COP31 kupitia wizara, idara na taasisi za Serikali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fursa zilizopatikana zinachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.