Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa kusimamia kikamilifu mikataba ya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana, akisisitiza utekelezaji wake ulete matokeo katika kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika nchini.

Agizo hilo limekuja wakati Tanzania ikipiga hatua katika sekta ya afya, baada ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 hadi 76, huku Rais Samia akitaka mafanikio hayo yawe msingi wa kuimarisha ajenda ya Afrika ya kutokomeza vifo vya wanawake na watoto ifikapo mwaka 2030.

1003898779-1024x683 Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Akizungumza leo Novemba 26,2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Kisayansi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe (RMNCAH+N), Rais Samia amesema Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zinapaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Katika mkutano huo, Serikali ilisaini mikataba mitatu, ukiwemo wa ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ kati ya Rais Samia na wakuu wa mikoa kwa ajili ya kusimamia mikakati ya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030.

1003898776-1024x705 Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Mkataba mwingine ulisainiwa na Kampuni ya Amsons Group kwa ajili ya ujenzi wa hospitali katika mikoa tisa, halmashauri 11 na Zanzibar.

Rais Samia amesema Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo vya uzazi kutoka 556 hadi 104 mwaka 2023, wakati ilipotunukiwa tuzo ya Goalkeepers Award na Gates Foundation, kabla ya kushuka zaidi hadi 76 katika takwimu za mwaka 2024/2025.

1003898774-1024x683 Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Pia, vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 24 hadi 17 na vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 43 hadi 28 kwa kila vizazi hai 1,000.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa uwekezaji katika huduma za afya, akibainisha kuwa Serikali imeongeza vituo vya afya na zahanati hadi 13,683, hospitali za wilaya kutoka 117 hadi 174 na hospitali za rufaa za mikoa kutoka 21 hadi 28.

1003898757-1024x582 Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Aidha, mfumo wa M-Mama umewezesha kusafirisha wagonjwa zaidi ya 250,000 hadi Agosti mwaka huu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wachanga.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Wizara imejipanga kuitumia nafasi ya Rais Samia kama Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Mama na Mtoto kuifanya Tanzania kuwa mfano na kitovu cha kujifunza kwa mataifa mengine ya Afrika.

1003898792-1024x576 Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Amesema Wizara imeweka utaratibu wa kila kifo cha mama na mtoto mchanga kuhesabiwa na kufanyiwa mapitio, huku taarifa zake zikifuatiliwa kitaifa kwa njia ya kidijitali.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Grace Maghembe amesema mkutano huo umejumuisha washiriki takribani 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wataalamu wa afya, watafiti, taasisi na vyuo.

1003898785-1024x576 Rais Samia aagiza mikataba ya afya kusimamiwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *