-Kuwaunganisha wananchi na matamasha, michezo, mikutano na shughuli mbalimbali nchini

Upatikanaji wa taarifa za matukio mbalimbali nchini unatarajiwa kuwa rahisi zaidi baada ya kutambulishwa kwa programu tumishi ya simu (App) iitwayo Kunani Tizii, inayolenga kuwaunganisha wananchi na taarifa za matukio yajayo na yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Programu hiyo inalenga kukusanya taarifa za matukio katika jukwaa moja la kidijitali, ikiwemo matamasha ya muziki, mashindano ya michezo, mikutano ya kibiashara, makongamano ya kidini, maonesho na shughuli za kijamii, ili kuwawezesha wananchi kuyatambua na kupanga ushiriki wao kwa wakati.
Kunani Tizii, ambayo tayari inapatikana kwa watumiaji wa simu za Android kupitia Google Play Store na tovuti yake, imeanzishwa kukabiliana na changamoto ya kutawanyika kwa taarifa za matukio katika majukwaa mbalimbali ya mawasiliano, hali inayosababisha baadhi ya wananchi kukosa fursa za kushiriki shughuli zinazoweza kuwa na manufaa kwao.
Akizungumzia ujio wa programu hiyo, Mkurugenzi wa Ubunifu wa Kampuni ya Empirical Communications, Samwel Gisayi, leo Novemba 16,2026, jijini Dar es Salaam, amesema wazo la kuanzisha jukwaa hilo limetokana na kubaini kuwa Tanzania ina matukio mengi yenye umuhimu wa kijamii na kiuchumi, lakini taarifa zake hazifiki kwa urahisi kwa watu wanaoweza kunufaika nayo.
“Tanzania haikosi matukio, bali kinachokosekana ni mfumo uliopangwa vizuri na unaofikika kwa urahisi utakaowawezesha watu kufahamu uwepo na ujio wa matukio hayo. Mkutano muhimu, tamasha au shughuli ya kijamii inaweza kufanyika bila kufahamika na watu ambao wangeweza kunufaika kwa kushiriki. Kunani Tizii imeanzishwa kutatua changamoto hiyo kwa kuwaunganisha waandaaji wa matukio na walengwa wao kupitia jukwaa moja,” amesema Gisayi.
Amefafanua kuwa tofauti na vyombo vya habari vinavyoripoti matukio baada au wakati yanapofanyika, Kunani Tizii inalenga zaidi kuwapatia wananchi taarifa za matukio yanayotarajiwa kufanyika ili waweze kujiandaa na kushiriki.
Amesema programu hiyo imeundwa kuhudumia maeneo tisa ya matukio, yakiwemo burudani, michezo, shughuli za Serikali na masuala ya umma, biashara, dini, elimu, maonesho, shughuli za kijamii na maendeleo ya jamii, pamoja na utalii na utamaduni.
Kupitia makundi hayo, watumiaji wataweza kupata taarifa za matamasha ya muziki, mechi za mpira wa miguu, mikutano ya kibiashara, makongamano ya kidini, maonesho ya kilimo, kampeni za afya na shughuli nyingine kulingana na maeneo na mambo wanayopendelea.
Kwa upande wa teknolojia, Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Empirical Communications na mtengenezaji wa programu hiyo, Gabriel Mlolwa, amesema jukwaa hilo limeundwa kwa vipengele mbalimbali vinavyorahisisha utafutaji na upatikanaji wa taarifa za matukio.
Amevitaja vipengele hivyo kuwa ni Happening Today (Matukio ya Leo), This Weekend (Matukio ya Mwishoni mwa Wiki), Free Events (Matukio ya Bure), Popular Events (Matukio Maarufu) na Coming Soon (Matukio Yajayo).
Aidha, amesema programu hiyo ina kipengele cha Near Me kinachomwezesha mtumiaji kutambua matukio yanayofanyika karibu na eneo alipo, pamoja na mfumo wa utafutaji unaomwezesha kuchagua matukio kulingana na maeneo na mambo anayoyapendelea.
“Katika utengenezaji wa programu hii, tulilenga kuhakikisha kuwa upatikanaji wa taarifa za matukio unakuwa rahisi. Mtumiaji hapaswi kulazimika kutembelea majukwaa mengi ili kupata taarifa za shughuli zinazomvutia. Kupitia vipengele kama utafutaji wa matukio kulingana na eneo, makundi ya matukio, kalenda na vikumbusho (reminders), tunarahisisha upatikanaji wa taarifa na maandalizi ya kushiriki,” amesema Mlolwa.
Ameongeza kuwa watumiaji wanaweza kushiriki taarifa za matukio wanazozipata kupitia WhatsApp, Instagram, Facebook, TikTok, X na barua pepe, ili kuwasaidia watu wengine kupata taarifa hizo.
Mbali na kuwahudumia wananchi, jukwaa hilo pia limelenga kuwapa waandaaji wa matukio fursa ya kutangaza shughuli zao na kuwafikia walengwa kwa urahisi zaidi.
Mlolwa alisema kupitia kipengele cha Organiser Dashboard, taasisi na waandaaji wa matukio wataweza kufungua akaunti na kuchapisha taarifa za shughuli zao, zikiwemo mabango, tarehe na maeneo ya kufanyika, majina ya wazungumzaji na wasanii, ratiba, taarifa za tiketi na viungo vya usajili.
Amesema mfumo huo unatoa fursa kwa vikundi vya kijamii, taasisi za dini na Serikali, kampuni binafsi pamoja na waandaaji wengine kutangaza matukio yao kupitia jukwaa moja, huku wafanyabiashara na kampuni wakipata nafasi ya kutangaza bidhaa na huduma zao.
Kuhusu upatikanaji wa tiketi, Mlolwa alisema Kunani Tizii inalenga kuunganisha taarifa za matukio na mifumo iliyopo ya utoaji tiketi pamoja na watoa huduma za malipo nchini, ili kurahisisha mchakato wa usajili na ununuzi wa tiketi kwa watumiaji.
Aidha, amesema kampuni hiyo inapanga kuanzisha utaratibu wa Kunani Tizii Weekend, utakaokuwa ukitoa orodha ya matukio 10 bora ya mwishoni mwa wiki kila Ijumaa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano.
Amesema kwa sasa wanaendelea na maandalizi ya kuanzisha toleo la programu hiyo kwa watumiaji wa simu za iOS, huku maboresho mengine yajayo yakitarajiwa kujumuisha mfumo wa kutoa tathmini na maoni kuhusu matukio na maeneo yanayotumika kuendeshea shughuli mbalimbali.
Amewahimiza Watanzania, wafanyabiashara, taasisi na waandaaji wa matukio kutumia jukwaa hilo kwa kupakua programu kupitia Google Play Store, kutembelea tovuti yake na kufuatilia kurasa zake za mitandao ya kijamii pamoja na chaneli ya YouTube.
“Tunalenga kuifanya Kunani Tizii kuwa jukwaa ambalo Watanzania watalitumia wanapohitaji kufahamu kinachoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ili kufanikisha hili, tunawaomba sana waandaaji wa matukio waitumie programu hii kusajili matukio yao bila kutozwa gharama yoyote, ili taarifa za matukio hayo ziwafikie walengwa wengi zaidi,” amehitimisha Mlolwa.