Washirika waendeleza ufadhili Nishati safi Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TANZANIA imepata ahadi mpya za ufadhili na uwekezaji kutoka kwa washirika wa maendeleo kwa ajili ya kuendeleza miradi ya nishati safi ya kupikia na nishati jadidifu, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa wananchi.

Ahadi hizo zimetolewa na taasisi mbalimbali za kimataifa na Serikali za nchi washirika kufuatia ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaoendelea jijini Antalya, Uturuki.

1003758222-1024x683 Washirika waendeleza ufadhili Nishati safi Tanzania

Waziri wa Nishati, Juma Zuberi Homera, amesema hayo Novemba 15, 2026, wakati akitoa taarifa ya ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Amesema miongoni mwa ahadi hizo ni Serikali ya Saudi Arabia kuendelea kufadhili miradi ya nishati, ikiwemo nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia.

Aidha, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha ufadhili wa majiko ya umeme 70,000, huku majiko mengine 70,000 yakitarajiwa kuidhinishwa hivi karibuni ili kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

1003758230-1024x688 Washirika waendeleza ufadhili Nishati safi Tanzania

Kwa upande wake, Shirika la UK Aid limeahidi kutoa pauni milioni nne kwa ajili ya miradi ya nishati safi ya kupikia na nishati jadidifu, pamoja na kuwezesha wananchi kupata majiko ya umeme kupitia mfumo wa malipo kidogo kidogo.

Vilevile, taasisi ya Sustainable Energy for All (SEforALL) imeahidi kushirikisha sekta binafsi kuunda muungano wa wawekezaji utakaohamasisha uwekezaji katika sekta ya nishati na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia.

Katika hatua nyingine, International Solar Alliance (ISA) imeahidi kushirikiana na Tanzania kuhamasisha matumizi ya nishati ya jua katika shule na vituo vya afya, pamoja na kutenga dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya miradi ya umeme wa jua katika nchi wanachama.

1003758235-1024x711 Washirika waendeleza ufadhili Nishati safi Tanzania

Mashirika mengine yaliyoahidi ushirikiano katika sekta hiyo ni Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA), Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Serikali ya Iceland.

Wizara ya Nishati imeeleza kuwa hatua inayofuata ni kuendeleza mazungumzo na wadau hao ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa zinageuzwa kuwa miradi ya maendeleo itakayochangia upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa wananchi.

1003758233-1024x644 Washirika waendeleza ufadhili Nishati safi Tanzania

Wakati huo huo, kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kimeongezeka kutoka asilimia 78.4 mwaka 2020 hadi asilimia 85.5.

Katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, taasisi 2,745 zinatumia nishati hiyo, huku mitungi 370,792 na majiko banifu 139,859 ikiwa imegawiwa kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *