Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasilisha mapendekezo matatu ya Tanzania kwa jumuiya ya kimataifa yanayolenga kuimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, yakijikita katika upatikanaji wa fedha za kutosha kwa nchi zinazoendelea, haki katika mpito wa nishati na kuendeleza uchumi jumuishi unaostahimili athari za tabianchi.
Rais Samia amewasilisha mapendekezo hayo leo Novemba 11, 2026, wakati akihutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika Antalya, nchini Uturuki, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa unaozingatia mahitaji na uwezo tofauti wa kila nchi.

Amesisitiza kuwa hatua za kukabiliana na changamoto hiyo zinapaswa kuzingatia haki na usawa, kwa kutambua tofauti za mazingira na hali za kitaifa.
“Hivyo ni lazima na ni muhimu kwamba hatua za tabianchi ziongozwe na usawa, haki ya tabianchi, na kanuni ya uwajibikaji wa pamoja lakini tofauti na uwezo wa nchi husika,” amesema.

Katika pendekezo la kwanza, ametaka nchi zinazoendelea kupata fedha za kutosha, zinazotabirika na zinazofikika, zikiwemo ruzuku na ufadhili wenye masharti nafuu, pamoja na uhamisho wa teknolojia na ujenzi wa uwezo.
Amesema Tanzania na nchi nyingine za Afrika zina fursa za kunufaika na uchumi wa kaboni kupitia sekta za usafirishaji, usimamizi wa taka, nishati ya maji, jotoardhi na upepo, pamoja na misitu inayofunika takribani hekta milioni 48.1 nchini.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa wazi wa soko la kaboni chini ya Kifungu cha Sita cha Makubaliano ya Paris ili kuhakikisha bei ya haki ya kaboni, mgawanyo wa faida wenye usawa na uadilifu wa kimazingira.
Katika pendekezo la pili, Rais Samia amesisitiza kuwekwa kwa haki ya nishati katika moyo wa mpito wa nishati duniani, akieleza kuwa Afrika inahitaji kuhakikisha wananchi wanapata nishati nafuu, ya kuaminika na endelevu.

Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mkataba wake wa taifa wa nishati kwa lengo la kupanua upatikanaji wa umeme nchini kote, hususan vijijini, huku akitoa wito wa kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, ufadhili wa bei nafuu na uhamisho wa teknolojia.
Pendekezo la tatu linahusu kuendeleza maendeleo jumuishi na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050 imeweka kipaumbele katika ubunifu, ukuaji wa viwanda na mabadiliko endelevu ya kiuchumi, yanayohitaji kuwajengea vijana stadi na kuwaandaa kupata ajira za kijani, pamoja na kupanua fursa katika nishati mbadala, kilimo endelevu na viwanda rafiki kwa mazingira.

“Tunajikita katika hatua za tabianchi zinazounda fursa kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kujitolea katika utekelezaji wa malengo ya Makubaliano ya Paris, huku akizitaka nchi zinazoshiriki COP31 kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa fedha, uhamisho wa teknolojia na ujenzi wa uwezo ili kuwezesha utekelezaji wa hatua za tabianchi.
Amesisitiza kuwa mkutano huo unapaswa kuhamisha dunia kutoka kwenye ahadi na makubaliano kwenda kwenye vitendo na matokeo yanayopimika.
“Wacha COP31 iwe kitovu cha mabadiliko kutoka ahadi kwenda kwenye utekelezaji, kutoka kwenye nia hadi vitendo, na kutoka kwenye makubaliano hadi matokeo yanayopimika,” amesema.
