Na Mwandishi Wetu, Iringa
WATU 21 wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa baada ya basi la abiria la kampuni ya Maokoto Bus Services kugongana na lori la mizigo katika ajali iliyotokea eneo la Njiapanda ya Kiponzero, barabara kuu ya Iringa–Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 9,2026 na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa imeeleza waliofariki ni wanaume 10, wanawake tisa na watoto wawili.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa majeruhi watano wamepata huduma za matibabu, huku mamlaka zikiendelea na taratibu za kushughulikia tukio hilo.Ilieleza basi hilo lilikuwa likitoka Kijiji cha Wasa, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kuelekea Iringa Mjini wakati lilipokumbwa na ajali hiyo.

Aidha, taarifa za awali zinahusisha chanzo cha ajali hiyo na hitilafu katika mfumo wa breki wa basi hilo, iliyodaiwa kusababisha dereva kushindwa kulidhibiti na hatimaye kugongana na lori.
Hata hivyo, chanzo rasmi cha ajali hiyo kitafahamika baada ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi kukamilika.