
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwawezesha wananchi kumiliki nyumba bora, salama na zinazokidhi mahitaji ya maisha ya sasa na yajayo, kupitia miradi ya nyumba za kisasa ikiwemo Mradi wa Saateni.
Dhamira hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati akizindua mauzo ya nyumba za kisasa za Mradi wa Saateni, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi, leo Novemba 8, 2026.

Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi na kupanua fursa za umiliki wa nyumba.
Dkt. Mwinyi amesema sekta ya makaazi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha watumishi wa umma, vijana, wafanyabiashara na wananchi wa kipato cha chini na cha kati kumiliki nyumba kwa masharti nafuu.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi ameelekeza familia zilizopisha maeneo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kuzingatiwa kwa kupatiwa nyumba maalum pamoja na punguzo la asilimia 50 ya kodi.
Amesema hatua hiyo inalenga kutambua mchango wa familia hizo katika kufanikisha mradi huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman, amesema Mradi wa Saateni unatarajiwa kuwa na jumla ya nyumba 209, maeneo ya biashara, huduma za kijamii na maegesho ya magari.

Amesema pia familia 25 zilizopisha eneo la mradi zimetengewa nyumba kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kufanikisha mradi huo.