*Lengo kuchochea akiba na uwekezaji
Na Mwandishi wetu
WIZARA ya Fedha imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi na wajasiriamali kupitia Awamu ya Nne ya Programu ya Elimu ya Fedha, inayolenga kuwawezesha kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Baadhi ya watumishi na wananchi wa Kata ya Lunyanywi, Wilaya ya Njombe Mji, mkoani Njombe, ni miongoni mwa wadau waliopata elimu hiyo kupitia filamu iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, ikifuatiwa na majadiliano yaliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Njombe Mji.

Katika zoezi hilo, wataalamu kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) walitoa elimu kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika kukuza kipato na kujenga utajiri, huku wataalamu kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakisisitiza umuhimu wa hifadhi ya jamii na maandalizi ya kifedha ya muda mrefu.
Washiriki pia walijadili masuala ya upangaji wa bajeti, utunzaji wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, usajili wa vikundi vya huduma ndogo za fedha na matumizi ya bima katika kulinda biashara na mali nyingine dhidi ya vihatarishi.

Utoaji wa elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Fedha na taasisi zake za kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma za kifedha na kuwajengea uwezo wa kutumia fursa za akiba na uwekezaji kwa manufaa yao.
Zoezi hilo lilishirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, CMSA, UTT AMIS na NSSF, kwa lengo la kuendeleza uelewa wa masuala ya fedha na kuchochea ustawi wa kiuchumi wa wananchi na jamii kwa ujumla.
