Visima vitatu vya Mnazi bay kuongeza akiba ya Gesi asilia

Na Salha Mohamed,Dar es Salaam

KUKAMILIKA kwa uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara ni hatua inayotarajiwa kuongeza akiba ya nishati hiyo nchini, ambayo kwa sasa inafikia futi za ujazo trilioni 57.54.

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema ugunduzi wa gesi asilia uliofanyika kupitia shughuli za uchimbaji katika kitalu hicho unatarajiwa kuongeza akiba iliyopo, huku Serikali ikitarajia kutangaza kiasi halisi cha gesi iliyogunduliwa wiki ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 18,2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Dkt. Homera amesema visima hivyo vinajumuisha viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti, vilivyochimbwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni ya M&P.

Amesema Serikali inatarajia kuzindua visima hivyo katika Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara, ambapo taarifa zaidi kuhusu kiasi cha gesi kilichogunduliwa zitatolewa.

Amesema ugunduzi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya nishati.Dkt. Homera amesema Serikali kupitia TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.

Ameeleza kuwa uchukuaji wa data za mitetemo unaendelea katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026.

Kuhusu Kitalu cha Ntorya, amesema maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha uzalishaji na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yanaendelea, huku ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka Ntorya hadi Madimba ukifikia asilimia 70.

Amesema mradi huo wa bomba unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kuanza mapema mwaka 2027 na kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku.

Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amesema TPDC inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi kusambaza gesi asilia majumbani na kwenye magari kupitia mfumo wa CNG, ambapo hadi Septemba 2026, vituo 22 vilikuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma.

Aidha, amesema wiki ijayo Serikali inatarajia kusaini na kukabidhi leseni mpya za utafutaji mafuta na gesi asilia (PSA) kwa TPDC ili kuliwezesha shirika hilo kuendelea na shughuli za utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali hizo. Makamu wa Rais, Dkt. Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

1003440061-1024x682 Visima vitatu vya Mnazi bay kuongeza akiba ya Gesi asilia
1003440063-1024x682 Visima vitatu vya Mnazi bay kuongeza akiba ya Gesi asilia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *