TFS Yaweka Wazi Fursa za Uwekezaji Sekta ya Misitu Mufindi

WhatsApp-Image-2026-10-16-at-09.28.16-1-1024x682 TFS Yaweka Wazi Fursa za Uwekezaji Sekta ya Misitu Mufindi

Na Mwandishi Wetu – Iringa

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia Shamba la Miti Sao Hill na Ofisi ya TFS Wilaya ya Mufindi, umetangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya misitu, ufugaji nyuki na utalii ikolojia katika Jukwaa la Uwekezaji na Maonesho la Mufindi (Mufindi Investment Forum & Expo 2026).

Maonesho hayo yamefunguliwa rasmi leo, Oktoba 16, 2026, mjini Mafinga, Wilaya ya Mufindi, na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, ambaye alitembelea banda la TFS na kupata maelezo kuhusu shughuli za wakala huo na fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za misitu na nyuki.

Dkt. Chaya ameipongeza TFS kwa kuwashirikisha wadau katika shughuli za uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Anaongeza kuwa jukwaa hilo si tukio la kuonesha bidhaa pekee, bali ni fursa ya kutangaza uwekezaji uliopo Mufindi, kujenga masoko, kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi, kukuza teknolojia na kuimarisha mahusiano ya kibiashara,” amesema.

Amesema kaulimbiu ya jukwaa hilo, Connect, Invest, Grow (Unganisha, Wekeza, Kuza), inasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutambua na kutumia fursa za uwekezaji kwa manufaa ya wananchi.

Dkt. Chaya ameitaka TFS kuendelea kushirikisha wadau katika shughuli zake na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha rasilimali za misitu na nyuki zinatumika kwa uendelevu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini, akieleza kuwa ubora ni miongoni mwa mambo muhimu yanayowezesha bidhaa za Tanzania kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema kufikiwa kwa malengo ya maendeleo kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zake, sekta binafsi, wawekezaji na wananchi, hivyo kuwataka wadau kutumia majukwaa kama hilo kuimarisha mahusiano na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, amesema wilaya hiyo inajivunia ukuaji wa uchumi unaochangiwa na shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo sekta ya misitu, ambayo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kiuchumi katika wilaya hiyo.

Jukwaa la Uwekezaji na Maonesho la Mufindi 2026 linafanyika kuanzia Oktoba 16 hadi 20, mjini Mafinga, likilenga kuwakutanisha wawekezaji na wadau mbalimbali ili kutangaza fursa za uwekezaji katika wilaya hiyo, zikiwemo misitu, ufugaji nyuki, utalii ikolojia na biashara ya mazao ya misitu.

WhatsApp-Image-2026-10-16-at-09.28.16 TFS Yaweka Wazi Fursa za Uwekezaji Sekta ya Misitu Mufindi
WhatsApp-Image-2026-10-16-at-09.28.15-1024x682 TFS Yaweka Wazi Fursa za Uwekezaji Sekta ya Misitu Mufindi
WhatsApp-Image-2026-10-16-at-09.28.13-1024x682 TFS Yaweka Wazi Fursa za Uwekezaji Sekta ya Misitu Mufindi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *