
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, amehimiza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao ili kuboresha utendaji kazi, kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wafanyabiashara.
Londo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), uliofanyika mkoani Morogoro, ambapo aliipongeza taasisi hiyo kwa hatua ilizochukua kuboresha Mfumo wa Huduma kwa Njia ya Mtandao (BRELA Online Services – BOS).
“Nimefurahishwa na hatua za BRELA katika kuboresha Mfumo wa BRELA Online Services (BOS), ambapo moduli tano kati ya saba zimeanza kutumika na ninawasisitiza kuendelea kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa utoaji huduma na kuboresha huduma kwa wananchi na wafanyabiashara,” amesema Londo.

Amesema Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia mahali pa kazi ili kuboresha utekelezaji wa majukumu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, ameitaka BRELA kuendelea kufanya mapitio na maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali kwa kushirikiana na wadau, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kurahisisha utoaji wa huduma nchini.
Ameongeza kuwa mchakato huo unapaswa kuwashirikisha wadau kikamilifu ili kupunguza urasimu, kuondoa masharti yanayokwamisha shughuli za biashara na kuimarisha uzingatiaji wa sheria.

Kwa upande wake, Elias Kalist, akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, amesema bodi hiyo inatambua na kuthamini jitihada zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuboresha utoaji wa huduma.
“Bodi ya Ushauri inaendelea kusisitiza umuhimu wa BRELA kutumia mifumo ya kidijitali, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha Wakala inachangia kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kukuza sekta binafsi na uwekezaji,” amesema Kalist.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027, wakala utaendelea kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa BRELA wa mwaka 2026/2027–2030/2031, kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kielektroniki, kukamilisha maboresho ya BOS, kuwezesha utoaji wa leseni za biashara za Kundi B kwa kushirikiana na mamlaka husika, pamoja na kuendelea kupitia sheria na kanuni mbalimbali kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
