
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
TUME ya Madini imewaagiza wamiliki wa leseni, mameneja na wakaguzi wa migodi kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, kwa lengo la kulinda maisha ya watu, mazingira na miundombinu.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, wakati akifunga mafunzo yaliyowakutanisha washiriki 510 mjini Kahama, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Mhandisi Swedi amesema maandalizi ya kukabiliana na mvua hizo yanapaswa kuzingatia hali halisi na vihatarishi vilivyopo katika kila mgodi, huku washiriki wakitakiwa kutekeleza maelekezo waliyopewa na kutumia maarifa hayo katika maeneo yao ya kazi.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, pamoja na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendelea kwa usalama.

Kwa mujibu wa Mhandisi Swedi, mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa na utayari wa wamiliki wa leseni, mameneja na wakaguzi wa migodi katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua kubwa.
Amesema mada zilizofundishwa zilihusu maandalizi ya kukabiliana na maafa, maeneo na miundombinu ya migodi inayoweza kuathirika, wajibu wa mameneja na wakaguzi, taratibu sahihi za uchimbaji pamoja na usalama na uimara wa miamba.
Mhandisi Swedi amewataka washiriki kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa maeneo na miundombinu ya migodi, kubaini vihatarishi mapema na kuhakikisha taratibu za kiutendaji na ukaguzi zinatekelezwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema Tume ya Madini itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukaguzi wa migodi, ikiwemo kusambaza vifaa vya kisasa katika mikoa ya kimadini.
Amesema vifaa hivyo vitasaidia kurahisisha ukaguzi na kubaini hali ya maeneo ya chini ya ardhi.
Aidha, amewataka wachimbaji wadogo kuimarisha usalama kwa kuweka kanuni ndogo na kufanya vikao kabla ya kuanza kila zamu ili kubaini idadi ya watu wanaoingia migodini.
Mhandisi Kamando amesisitiza kuwa wakati wa mvua, watu hawapaswi kuruhusiwa kuingia katika mashimo yenye vihatarishi vya usalama.
“Wakaguzi wa madini, kama kuna kipindi hamtakiwi kulala ni hiki. Kama duara ni bovu, msioneane haya kusema ukweli. Mmiliki wa duara akikaidi na kupeleka watu, hatua stahiki zichukuliwe,” amesema.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Madini, Francis Kayichile, amewataka wachimbaji kuzingatia sheria, kanuni na masharti ya leseni zao.
Amesema kila leseni ya uchimbaji ina masharti ambayo mwenye leseni anatakiwa kuyatekeleza, akionya kuwa kutotekeleza masharti hayo kunaweza kusababisha hatua za kisheria.
“Shimo likipata shida wakati mlishatahadharishwa, sheria itawabana na hatutafumbia macho,” amesema Kayichile.
