
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MJANE wa Mkuu wa Mkoa wa kwanza wa Shinyanga, Casian Mikullo Kapilima, Mariam Mongi (86), amedai kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa siku mbili kufuatia agizo alilodai lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika mgogoro wa umiliki wa eneo lenye ukubwa wa ekari 10 lililopo Madale, Kinondoni.
Mongi, ambaye ni miongoni mwa wanaodai kumiliki eneo hilo, amesema familia yao haikupokea taarifa rasmi ya kuitwa katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro huo kabla ya kutolewa kwa agizo la kuwatafuta kwa madai ya kutotii wito.
Akizungumza Septemba 23, 2026, baada ya kuachiwa, Mongi amesema alikamatwa kufuatia agizo alilodai lilitolewa Septemba 19, wakati Mkuu wa Mkoa alipofika katika eneo linalogombaniwa.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa familia hizo, Wilson Ogunde, watu watano, wakiwamo wanawake wawili na vijana watatu, walifika kwa hiari baada ya kupata taarifa kuhusu agizo hilo, lakini walichukuliwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay ambako walishikiliwa.
Ogunde amesema miongoni mwa waliokamatwa ni Mongi mwenye umri wa miaka 86, ambaye, kwa mujibu wake, anahitaji huduma maalum za afya.
Amedai kuwa waliokamatwa wote waliachiwa bila kufikishwa mahakamani wala kufunguliwa mashtaka.
MGOGORO WA MUDA MREFU
Ogunde amesema familia hizo zimekuwa zikishiriki katika vikao mbalimbali vya kutafuta suluhu ya mgogoro huo, huku akidai kuwa zimepata ushindi katika baadhi ya hatua za kimahakama kuhusu umiliki wa eneo hilo.
Kwa msingi huo, amesema kinachohitajika sasa ni Serikali kuchunguza kiini cha mgogoro huo kwa kina ili kubaini uhalali wa madai ya kila upande na kuhakikisha maamuzi halali ya vyombo vya sheria yanazingatiwa.
Ameiomba Serikali, kupitia Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati suala hilo kwa kuhakikisha mgogoro huo unapata suluhu ya haki, pamoja na kuchunguza madai ya watu wanaodaiwa kuuza maeneo yenye migogoro.
“Tunaiomba Serikali ijikite katika kiini cha mgogoro na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote, badala ya kutumia nguvu dhidi ya watu wanaodai kuwa na umiliki halali uliothibitishwa na mahakama,” amesema Ogunde.
