
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Tanzania itatumia mashindano ya Miss World 2027 yatakayofanyika nchini kama fursa ya kujitangaza zaidi kimataifa na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani.
Makonda amesema hayo leo, Septemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu aliouandaa, akieleza kuwa Serikali imekusudia kutumia mashindano hayo kutangaza utamaduni, lugha na vivutio mbalimbali vya Tanzania.
Amesema kila taifa litakaloshiriki mashindano hayo litatakiwa kutunga wimbo ambao utatafsiriwa kwa Kiswahili, hatua ambayo amesema itasaidia kueneza lugha hiyo katika mataifa mbalimbali duniani.
“Mashindano ya Miss World yatakayofanyika hapa Tanzania yatakuwa na mambo mengi, na moja ya lengo kubwa la Serikali chini ya Dkt. Samia ni kutumia kila aina ya fursa kuitangaza nchi yetu ili wageni waje wajenge uchumi,” amesema Makonda.
Amesema kupitia mashindano hayo Tanzania inalenga kutumia fursa mbalimbali zitakazojitokeza kujitangaza kimataifa, kuvutia wageni na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.
Makonda amesema maandalizi ya mashindano hayo yanapaswa kwenda sambamba na mkakati wa kuhakikisha Tanzania inanufaika na fursa za kiutamaduni, utalii na kiuchumi zitakazotokana na ujio wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali.