Tanzania mbioni kuanza uchimbaji wa chuma, mitambo ya kisasa yawasili Maganga Matitu

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA ipo katika hatua za mwisho za kuandika historia mpya ya maendeleo ya sekta ya madini na viwanda baada ya mitambo mikubwa ya kisasa ya uchimbaji madini ya chuma kuwasili nchini ikiwa njiani kwenda eneo la Mradi wa Maganga Matitu uliopo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Limited (Fujian) ambapo utahusisha uchimbaji wa madini ya chuma katika eneo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 19, pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata chuma ghafi.

Akizungumza mara baada ya kuwasili kwa mitambo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, amesema hatua hiyo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inaanza kuchimba na kunufaika kikamilifu na rasilimali
zake za madini ya chuma.

1-31-1024x768 Tanzania mbioni kuanza uchimbaji wa chuma, mitambo ya kisasa yawasili Maganga Matitu
Baadhi ya mitambo ambayo tayari imewasili kwa ajili ya uchimbaji na uchenjuaji wa Chuma katika mradi wa Maganga Matiti

“Kuwasili kwa mitambo hii ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa mradi ambao utabadilisha historia ya sekta ya madini ya chuma nchini. Zaidi ya Dola za Marekani milioni 70 zinawekezwa katika mradi huu ambao utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla,” amesema Dkt. Shombe.

Dkt Shombe amesisitiza kuwasili kwa mitambo hiyo ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa mradi ambao utabadilisha historia ya sekta ya madini ya chuma nchini.

Amesema utekelezaji wa mradi huo utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla ambapo kwa sasa Tanzania inatumia zaidi ya dola bilioni 1.22 (zaidi ya sh. trilioni 3.2) kununua bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi na kwamba sekta hiyo inashika nafasi ya pili kwa matumizi makubwa ya fedha za kigeni (baada ya mafuta).

Ameongeza NDC itaendelea kushirikiana kwa karibu na kampuni ya Fujian kuhakikisha ndoto ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya chuma inakuwa uhalisia.

2-25-1024x768 Tanzania mbioni kuanza uchimbaji wa chuma, mitambo ya kisasa yawasili Maganga Matitu
Baadhi ya mitambo ambayo tayari imewasili kwa ajili ya uchimbaji na uchenjuaji wa Chuma katika mradi wa Maganga Matiti

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundindi, Steven Sapi Mlewa, amesema wananchi wamepokea ujio wa mradi huo kwa matumaini makubwa kutokana na fursa za ajira na biashara zitakazozalishwa.

“Kwa miaka mingi tulikuwa tunasikia kuhusu Mradi wa Maganga Matitu, lakini leo tunaona utekelezaji wake kwa vitendo. Kuwasili kwa mitambo kunatupamatumaini mapya ya ajira kwa vijana, kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi wa wananchi wetu,” amesema.

Pia Meneja wa Mradi, Mhandisi Wallu Kapaya, amesema Mradi wa Maganga Matitu unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuongeza uzalishaji wa malighafi muhimu kwa viwanda, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha sekta nyingine zinazotegemea shughuli za uchimbaji.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku pia ukichochea maendeleo ya miundombinu ikiwemo barabara, huduma za jamii, biashara na uwekezaji katika maeneo yanayouzunguka.

Lakini pia Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mundindi, Adrat Msigwa, alisema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa mradi na namna ya kutumia fursa zitakazojitokeza.

“Wananchi wamekuwa na ushirikiano mkubwa. Tunaendelea kuwahamasisha kujiandaa kunufaika na ajira, biashara ndogo ndogo pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali zitakazotokana na mradi huu,” amesema.

Wananchi waonesha matumaini makubwa

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mundindi, wamesema utekelezaji wa mradi huo unaashiria mwanzo wa zama mpya za maendeleo katika eneo hilo.Mkazi wa Mundindi, Jonisia Mlowe, amesema vijana wengi wamekuwa wakihama kwenda mikoa mingine kutafuta ajira, lakini sasa wana matumaini ya kupata ajira karibu na makazi yao.

“Tunafurahi kuona mradi umeanza kwa vitendo. Tunaamini vijana wengi sasa watapata ajira hapa nyumbani badala ya kuhangaika kwenda mbalikutafuta maisha,” amesema.

3-22-1024x768 Tanzania mbioni kuanza uchimbaji wa chuma, mitambo ya kisasa yawasili Maganga Matitu

Kwa upande wake, mfanyabiashara Moses Mwakalinga, amesema ongezeko la shughuli za mradi litafungua fursa nyingi za biashara ambapo matarajio yao ni kuona vijana wa maeneo yanayouzunguka mradi wakipewa kipaumbele katika ajira na mafunzo ya ujuzi.

“Kadri shughuli za mradi zitakavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya chakula, malazi, usafiri na huduma nyingine yatakavyoongezeka, jambo ambalo litaongeza kipato cha wananchi,” amesema.

Ujenzi wa mradi kukamilika ndani ya miaka miwili

Mbali na kuwasili kwa mitambo ya uchimbaji, maandalizi mengine muhimu yanaendelea ambapo TANESCO tayari imeanza kazi ya kusambaza umeme kwa kujenga miundombinu ya nguzo kuelekea eneo litakapojengwa kiwanda cha uchakataji wa madini ya chuma.

Ujenzi wa mradi unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili, hatua itakayowezesha Tanzania kuanza kunufaika na rasilimali zake za madini ya chuma kwa kiwango kikubwa zaidi.

Mradi huu unatekelezwa na NDC akiwa ni mwekezaji wa kimkakati kwa niaba ya Serikali akishirikiana na mbia mwenza wa sekta binafsi Kampuni ya FUJIAN.

5-3-1024x768 Tanzania mbioni kuanza uchimbaji wa chuma, mitambo ya kisasa yawasili Maganga Matitu

Uwekezaji huu ni wa kimkakati na una mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 hususani katika uendelezaji wa rasilimali za kimkakati na zenye masilahi makubwa ya kiuchumi kwa Maendeleo ya Taifa letu Uhakiki wa taarifa za mashapo uliofanyika katika mradi huu wa Maganga Matitu umeonesha uwepo wa mashapo ya chuma tani milioni 101.

Mradi huu ni wa pili kwa ukubwa nchini ukifuatia Mradi Mkubwa wa Kitaifa wa Liganga wenye mashapo ya chuma zaidi ya Tani zaidi milioni 126.

Kuwasili kwa mitambo hiyo kunathibitisha kuwa ndoto ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya chuma sasa imeanza kutimia, huku Maganga Matitu ikijiandaa kuwa kitovu kipya cha maendeleo ya uchumi na viwanda nchini.

Mradi wa Maganga Matitu unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa malighafi za chuma kutoka nje ya nchi, kuongeza mapato ya Serikali na kufungua maelfu ya fursa za ajira na biashara kwa wananchi.

6-1024x768 Tanzania mbioni kuanza uchimbaji wa chuma, mitambo ya kisasa yawasili Maganga Matitu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *