Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema imekamilisha rasimu ya sheria na kanuni za kusimamia matumizi ya fedha za kidijitali nchini, hatua inayolenga kuweka mfumo madhubuti wa kulinda watumiaji wa huduma za kifedha na kudhibiti matumizi mabaya ya teknolojia hiyo.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Emmanuel Tutuba, amesema hatua hiyo inahusisha usimamizi wa mali za kidijitali ikiwemo Bitcoin na Stablecoins, ambazo matumizi yake yanaongezeka duniani pamoja na kuibua changamoto mbalimbali za kiusalama na kifedha.
Akizungumza alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Tutuba amesema rasimu hizo sasa zitafuata hatua za kisheria kabla ya kuanza kutumika.

“Tunaendelea kukamilisha maandalizi ya sheria na kanuni za usimamizi wa fedha za kidijitali. Concept note imeshakamilika, rasimu ya sheria na rasimu ya kanuni pia zimekamilika. Sasa zitapelekwa katika vyombo vinavyohusika kwa hatua nyingine za kisheria,” amesema Dkt.Tutuba.
Amefafanua kuwa mchakato huo utahusisha Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Baraza la Mawaziri na hatimaye Bunge, huku maoni ya wadau yakipokelewa kabla ya sheria hizo kupitishwa.
Dkt. Tutuba amesema BoT imeamua kulichukua suala hilo kwa umakini kutokana na ongezeko la matumizi ya fedha za kidijitali, huku baadhi ya wananchi, hususan vijana, wakianza kuwekeza katika mali hizo bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu hatari zake.
“Kuna vijana wanawekeza huko lakini pia kuna malalamiko ya wengine kupoteza fedha. Ndiyo maana tunataka kuweka mfumo utakaoifanya shughuli hiyo ifanyike kwa usalama zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya fedha hizo za kidijitali zimekuwa zikitumika katika utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi, hali inayolazimu kuwepo kwa sheria na kanuni madhubuti zitakazolinda mfumo wa kifedha wa nchi.
Aidha, amesema BoT imejifunza uzoefu wa mataifa mbalimbali katika usimamizi wa fedha za kidijitali, ikiwemo kupitia mjadala uliofanyika katika mkutano wa magavana wa benki kuu duniani uliofanyika nchini Uswisi.
“Tunataka sheria itakayokidhi mahitaji ya Tanzania lakini pia iendane na viwango vya kimataifa ili kulinda watumiaji wa huduma za kifedha na mfumo mzima wa uchumi,” amesema.
Dkt. Tutuba amesisitiza kuwa lengo la BoT si kuzuia maendeleo ya teknolojia ya fedha, bali kuhakikisha matumizi yake yanafanyika katika mazingira salama yanayolinda wananchi na uchumi wa Taifa.
