
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema katika mwaka huu wa fedha linatarajia kuunganisha zaidi ya nyumba 2,600 na huduma ya gesi asilia ya kupikia katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Mtwara, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Masoko wa TPDC, Neema Cleophace, amesema zaidi ya nyumba 1,000 zitaunganishwa Dar es Salaam, zaidi ya nyumba 800 katika Wilaya ya Mkuranga na nyingine zaidi ya 800 katika Mkoa wa Mtwara.
Cleophace amesema TPDC inaendelea na jitihada za kuongeza matumizi ya gesi asilia nchini, hususan katika sekta ya kupikia, ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kutumia nishati safi na salama.
Amesema gesi asilia inayotumika nchini inapatikana katika mikoa ya Mtwara na Lindi na ina matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani, kwenye magari, viwandani na katika uzalishaji wa umeme.
Kwa mujibu wake, takribani asilimia 70 ya gesi asilia inayozalishwa nchini hutumika kuzalisha umeme, huku TPDC ikiwa tayari imeunganisha zaidi ya nyumba 2,500 kutumia gesi asilia kwa matumizi ya majumbani.
Aidha, amesema zaidi ya magari 5,000 tayari yanatumia gesi asilia, yakihudumiwa na vituo zaidi ya 18 vya kujazia gesi asilia nchini, huku zaidi ya viwanda 59 vikilitumia katika shughuli za uzalishaji kutokana na faida zake za kupunguza gharama za nishati na kuongeza ufanisi.
Amewataka wananchi kutembelea banda la TPDC katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu matumizi na faida za gesi asilia pamoja na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo.

