Na Salha Mohamed
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha VETA Dakawa mkoani Morogoro imetumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuhamasisha wananchi kutumia fursa ya uzalishaji wa sumu ya nyuki, ikieleza kuwa ni zao lenye thamani kubwa linalotumika kutengeneza dawa za binadamu na vipodozi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkufunzi kutoka VETA Dakawa, Theodora Kiyungu, alisema chuo hicho kimeleta ubunifu wa mzinga wa kisasa pamoja na mashine ya kuvunia sumu ya nyuki kwa lengo la kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo katika ufugaji wa nyuki.
Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na misitu mingi inayofaa kwa shughuli za ufugaji wa nyuki, jambo linalotoa fursa kubwa za uzalishaji wa mazao mbalimbali yatokanayo na nyuki, ikiwemo sumu ya nyuki.
“Mzinga huu umeunganishwa na kifaa maalumu kinachotumia umeme wa kuchaji kwa ajili ya kuvuna sumu ya nyuki. Kifaa hiki kina paneli na sehemu ya kioo yenye nyaya zinazopitisha umeme wa volti 10, ambazo huwekwa katika mlango wa mzinga,” amesema Kiyungu.

Ameeleza kuwa nyuki anaporudi kutoka kutafuta chakula hugusa nyaya hizo na kupata shoti ndogo isiyomdhuru, hali inayochochea utoaji wa sumu ambayo hukusanywa kwa ajili ya kuvunwa.
Kiyungu amesema kifaa hicho huwekwa kwenye mzinga kwa muda wa nusu saa, kisha hutolewa na sumu ya nyuki huvunwa.
Amesema sumu ya nyuki ni zao lenye thamani kubwa kwa kuwa hutumika kutengeneza dawa zinazotumika hospitalini pamoja na vipodozi, hivyo ni fursa muhimu ya kuongeza kipato kwa wafugaji wa nyuki.
Amefafanua kuwa VETA Dakawa imeamua kutumia Maonesho ya Sabasaba kutoa elimu hiyo baada ya kubaini kuwa wafugaji wengi wamekuwa wakijikita katika mazao mawili pekee ya nyuki, ambayo ni asali na nta, huku wakisahau mazao mengine yenye thamani kubwa kiuchumi, ikiwemo sumu ya nyuki.
Hata hivyo, amewashauri wananchi kujifunza ufugaji wa nyuki kupitia VETA Dakawa, akibainisha kuwa chuo hicho kwa sasa kinatoa pia kozi ya ufugaji wa nyuki kwa njia ya mtandao ili kuwafikia watu wengi zaidi.
“Mimi, Theodora Kiyungu, nimefanya ubunifu wa mzinga huu, halafu mashine ya kuvunia sumu ya nyuki imebuniwa na mtaalamu mwingine,” amesema Kiyungu.
