Na Salha Mohamed
Wanafunzi wanaosoma mkondo wa elimu ya amali wamekuwa kivutio katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) baada ya kuonesha ujuzi wa vitendo katika fani mbalimbali, hatua inayodhihirisha mafanikio ya maboresho ya mtaala wa elimu nchini.
Kupitia banda la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), wanafunzi hao wameonesha uwezo katika kazi za umeme, uchoraji wa ramani za majengo na ubunifu wa miradi mbalimbali, huku wakithibitisha kuwa elimu ya amali inawaandaa vijana kujiajiri na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 2, 2026, Kaimu Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa NACTVET, Dora Tesha, alisema maonesho hayo yamekuwa fursa ya kuwafikia wananchi, wazazi na wadau mbalimbali kwa kuwapa elimu kuhusu nafasi ya elimu ya amali pamoja na majukumu ya baraza katika kusimamia ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Alisema NACTVET ina jukumu la kuhakikisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi vinatoa mafunzo yanayozingatia viwango vinavyokubalika na kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Tesha alisema banda la NACTVET linatoa huduma mbalimbali zikiwemo taarifa kuhusu usajili wa vyuo, haki za wanafunzi na elimu kuhusu mkondo wa amali ulioanzishwa kupitia maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023.
“Tumewaleta wanafunzi kwenye maonesho haya ili wazazi na wananchi wajionee uwezo wao. Wapo wanaofanya kazi za umeme, kuchora ramani za majengo na kutengeneza miradi mbalimbali. Haya ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa kwenye elimu ya amali,” alisema Tesha.
Mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kutoka Shule ya Sekondari Baobab,Kidato cha tatu anayesomea fani ya umeme Careen Jonathan Maky alisema mkondo huo umemjengea uwezo wa vitendo na kumpa matumaini ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi.
Kwa upande wake, Mwalimu wa taaluma ya amali katika Shule ya Sekondari Baobab, Philip Lazaro, alisema mfumo huo unawajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kuanzisha biashara zao badala ya kusubiri ajira rasmi baada ya kuhitimu masomo.

Pia mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Wavulana Bwiru, Kidato cha tatu, Daud Elias, alisema mafunzo ya amali yamemwezesha kujifunza kuchora ramani za majengo na kuelewa hatua mbalimbali za ujenzi, akieleza kuwa kuendelea kuimarishwa kwa mkondo huo kutazalisha vijana wengi wenye ujuzi watakaochangia maendeleo ya uchumi wa taifa.