Na Salha Mohamed
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amekutana na kufanya Mdahalo wa kiuchumi na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo mkoani Morogoro, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo kuhusu dhana nzima ya ubia na nafasi yake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akizungumza katika mhadhara huo,Kafulila ameeleza ushiriki wa vijana, hususan wanafunzi wa vyuo vikuu, ni muhimu katika kufanikisha agenda ya maendeleo ya nchi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Amesema mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ni moja ya nyenzo muhimu za kuchochea uwekezaji, kuboresha utoaji wa huduma na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.
Kwa upande wao, wanafunzi walioshiriki mdahalo huo, wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema kuwa itawasaidia kuelewa fursa zilizopo na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Mhadhara huo,ni sehemu ya jitihada za PPP Centre za kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu umuhimu wa ubia katika maendeleo endelevu ya Tanzania.

